SIKU chache baada ya Jeshi la Polisi kumuua kinyama mwandishi wa
habari wa kituo cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, baadhi ya askari
waaminifu wamefichua siri za mauaji yanayofaywa na jeshi hilo. Wakizungumza na Tanzania Daima kwa sharti la kutotajwa majina yao
gazetini, askari hao walisema wakuu wao wanatumiwa kwa amri za watawala
ili kuingilia kudhibiti matukio ambayo wakati mwingine husababisha
vurugu zinazopoteza uhai wa wananchi.
Walisema tatizo kubwa ni wakuu wa polisi wilaya (OCD), makamanda wa
mikoa (RPC) na maofisa upelelezi wa mikoa (RCO) ambao hulazimishwa
kufanya kazi kwa amri ya wakuu wa wilaya na mikoa.
“Hawa wakuu wa wilaya na mikoa ni viongozi wa chama tawala, CCM.
Hivyo, ili viongozi wetu wa polisi waweze kupanda vyeo ni lazima
wajipendekeze kwao; yaani hata kipindi cha kampeni mkuu wa wilaya anampa
amri OCD kudhibiti wapinzani,” alisema mmoja wa askari hao. Walifafanua kuwa ili tatizo hilo liweze kuisha na jeshi hilo kufanya
kazi kwa mujibu wa sheria na uhuru, ni lazima vyeo hivyo vya wakuu wa
wilaya na mikoa vifutwe kwenye katiba mpya ijayo.
Mwangosi aliwashtukia askari
Naye Mkuu wa Operesheni ya M4C ya CHADEMA, Benson Kigaila, jana
alifichua siri mjini Iringa, akisema kuwa Mwangosi aliwatilia shaka
mapema polisi waliokuwa kwenye tukio hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Kigaila alisema kuwa muda mfupi
kabla ya kuuawa kwake, Mwangosi alimweleza kuwa askari wengi
anaowafahamu si wale waliokuwa eneo la tukio kudhibiti mkusanyiko wa
CHADEMA. “Marehemu aliniambia kuwa hapa nina shaka na hawa polisi kwa kuwa
wengi ninawafahamu lakini ninaowaona si wale ninaowafahamu.Wanaofanya
kazi za jeshi ni mamluki wasio na mafunzo,” alisema Kigaila.
Wakati siri hiyo ikifichuliwa, taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo
mkoani Iringa zinadai baadhi ya askari wanaodaiwa kumuua Mwangosi
wamekamatwa kwa siri na kuwekwa chini ya ulinzi.
Chanzo chetu kinasema kuwa jeshi hilo mkoani Iringa tangu juzi
linahaha kuchukua hatua za dharura za kuwafundisha askari wake matumizi
sahihi ya silaha wakati wa kutuliza ghasia.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa tayari askari watano kati ya saba
walioonekana kwenye picha mbalimbali za magazeti na mitandao wakimpiga
Mwangosi, wametiwa mbaroni.
“Hili suala limetuweka katika wakati mbaya sana na hivi ninavyoongea
na wewe tayari askari watano kati ya saba wanashikiliwa katika kituo cha
polisi Mufindi, lakini habari hizi zinafanywa siri sana,” kilisema
chanzo chetu.
Miongoni mwa askari watatu ambao hawajakamatwa kwa mujibu wa chanzo
hicho, ni pamoja na yule anayeonekana katika picha mbalimbali akiwazuia
wenzake waliomzunguka Mwangosi kwa kunyoosha mkono juu na na baadae
akiwa amejeruhiwa.
Mbali na askari huyo anayetambulika kwa jina moja la Mwampamba, pia
yule anayeonekana pichani akiwa ameshikilia silaha aina ya bastola
anayetajwa kwa jina la Gabriel, naye hajakamatwa.
Habari zaidi zinaeleza kuwa askari wengi waliokuwa katika operesheni
hiyo siku ya tukioa eneo la Nyololo, hawakuwa na mafunzo sahihi ya
kutumia mabomu ya machozi.
“Kiutaalamu mabomu ya machozi yanatakiwa yalengwe juu na kuwe na
umbali wa mita 60 mpaka 120, lakini ikitumika kinyume chake yanaweza
kudhuru au kuua.
“Katika kutuliza ghasia kuna mabomu ya aina mbalimbali ambayo
yanatakiwa kutumiwa kulingana na wakati, mabomu hayo ni yenye moshi
mzito, mwepesi na rangi ambayo lengo lake ni kuwaweka alama watu
watakaokuwa katika kundi linalotakiwa kudhibitiwa ili waweze
kujulikana,” kilibainisha chanzo hicho.
Kwamba askari wengi wa usalama barabarani siku hiyo walikuwa ni
wanawake kwani wale wa kiume wote walitakiwa kuvaa nguo za Kikosi cha
Kuzuia Fujo (FFU).
Habari hizo zinaongeza kuwa, kutokana na hali hiyo maafisa wa jeshi
hilo walilazimika kutoka jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kwenda Iringa
kutoa mafunzo kwa askari wa mkoa huo juu ya matumizi sahihi ya silaha.
Alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa askari hao wanaotuhumiwa kuua,
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, alikataa
kuzungumzia suala hilo akisema limeshaundiwa tume.
“Hizo taarifa mimi sina na siwezi kuzungumzia suala hilo kwa kuwa
limeshaundiwa tume. Tusubiri majibu yake, lakini hilo la kuja kwa
maofisa kwa ajili ya kutupatia mafunzo mimi sijui, wewe umezipata wapi?”
alisema Kamuhanda.
chanzo gazeti la Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment