INADAIWA
kwamba askari waliokuwa katika operesheni ya kuzuia mkutano wa Chadema
katika eneo la Nyololo wilayani Mufindi, Iringa na ambayo ilisababisha
kifo cha Mwandishi wa Habari, Daudi Mwangosi walitolewa katika mikoa ya
Dodoma, Morogoro na Mbeya.
Tayari tukio hilo limeibua mjadala
mzito kiasi cha kumfanya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel
Nchimbi kuunda tume huru kubaini chanzo cha tukio hilo. Marehemu
Mwangosi alizikwa juzi nyumbani kwao Tukuyu, mkoani Mbeya.
Habari
za uhakika zilizolifikia gazeti hili jana zilisema kuwa polisi hao
kutoka mikoa hiyo mitatu wakiwa wamesheheni vifaa mbalimbali likiwamo
gari la maji ya kuwasha, walisafiri siku moja kabla ya mkutano huo wa
Chadema na baadaye kuzuka vurugu zilizosababisha kifo hicho.
Marehemu Mwangosi aliuawa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni wa bomu ambao ulisambaratisha vibaya sehemu kubwa ya mwili wake.
Chanzo
cha habari kutoka mkoani Dodoma kilisema: “Hapa kwetu kuna askari 10 na
tunawafahamu kwa majina. Waliondoka hapa siku moja kabla ya tukio hilo
wakiwa na gari la washawasha.”
Chanzo hicho kilisema kwamba awali,
hawakuwa wakifahamu kama baadhi ya wenzao walichukuliwa na kupelekwa
Iringa. “Tulikuja kuona kwenye gazeti picha na tulipofuatilia tukaelezwa
kuwa ni kweli Dodoma ilitoa askari kwenda Iringa.”
Askari
mwingine aliyekuwa katika operesheni hiyo ambaye jina lake tunalihifadhi
kwa sababu za kitaaluma, alikiri kuwa hadi jana baadhi yao walikuwa
bado wako Iringa na kwamba walikwenda kwa agizo la wakubwa wake wa kazi.
“Sisi
ni Watanzania, lakini tumelazimika kuyafanya hayo kwa sababu ya mkate
(malipo). Kwa kweli haikuwa haki, kuwatoa askari na silaha kutoka mikoa
mitatu kana kwamba wanakwenda kupigana vita!”
Alidokeza kwamba,
askari wote waliotoka Dodoma walikuwa njiani kurudi mkoani humo, jana
lakini gari la maji ya kuwasha liliendelea kubaki huko Iringa likiwa na
dereva wake na askari mmoja mwenye cheo cha inspekta. Askari huyo
alisema kwamba gari hilo lililazimika kubaki kutokana na hitilafu.
“Wengine
wamerudi lakini, kuna wengine wenye gari la kuwasha bado walikuwa
Iringa, gari lao limepata hitilafu kidogo,” kilisema chanzo hicho kutoka
mjini Dodoma.
Mmoja wa askari hao alidaiwa kwamba hiyo inaweza
kuwa moja ya sababu ya askari hao kumshambulia marehemu Mwangosi wakati
mwenzao anayemfahamu akijaribu kuwazuia. "Hii inaonyesha kuwa askari hao
waliompiga walikuwa hawamjui na huyu aliyekuwa akiwazuia, alimjua.”
No comments:
Post a Comment