KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk.
Willibroad Slaa, amemvaa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais
Jakaya Kikwete, akisema amekitengenezea kaburi la kukizika rasmi chama
chake kwa kuruhusu watuhumiwa wakubwa wa ufisadi kugombea nyadhifa
mablimbali.
Dk. Slaa alisema uteuzi wa wagombea ndani ya CCM uliomalizika juzi
umeonyesha wazi kwamba sasa chama hicho kinatumbukia kwenye dimbwi kubwa
na pana lisiloweza kukitoa tena.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Mwanza, alikojichimbia
kuhakikisha mchakato wa uchaguzi wa mameya wa jiji hilo unakwenda vizuri
leo, Dk. Slaa alisema dhamira ya kweli dhidi ya CCM katika kuwaweka
vijana kwenye uongozi ili kukinusuru chama hicho imezimika baada ya
Kikwete kuruhusu watuhumiwa wa ufisadi na wakongwe kugombea uongozi.
“Katika hili la uteuzi wa CCM, nangojea taratibu zao zikamilike.
Tulitegemea CCM muda huu ni wa kujisafisha, lakini imeshindwa kufanya
hivyo. Mimi simung’unyi maneno kuhusu watuhumiwa wa ufisadi.
Mfano (anataja) ni fisadi wa fedha za rada. Mimi hapa nilishapeleka
ushahidi hadi wa akaunti namba ya benki yake kwa DPP (Mkurugenzi wa
Mashtaka Nchini), alisema.
Alisema inashangaza kuona katika utetezi wa CCM, mtuhumiwa huyo
amepatiwa nafasi licha ya kushindwa kueleza wazi fedha nyingi kwenye
akaunti hiyo ya Uswisi alizipataje.
“Mtuhumiwa mkubwa kama huyu wa ufisadi eti leo CCM inampitisha awe
mgombea. Kweli? Sioni dhamira ya CCM kupambana na vitendo vya kifisadi.
Na hata dhamira ya vijana haipo bali imejitumbukiza kwenye dimbwi ambalo
kamwe hakitatoka humo,” alisisitiza.
Kuhusu Lowassa na tuhuma zake za ufisadi wa kampuni ya kufua umeme wa
dharura wa Richmond zilizosababisha kujiuzulu uwaziri mkuu mwaka 2008,
Dk. Slaa alisema kiongozi huyo alilazimika kujiuzulu kama sehemu ya
kuwajibika, lakini ameshindwa hadi leo kumtaja mhusika hasa wa kampuni
hiyo.
Alisema kama kweli Lowassa alisingiziwa katika tuhuma hizo, alipaswa
kuwaeleza Watanzania nani anayehusika na ufisadi huo wa Richmond ambayo
ilishindwa kuzalisha umeme licha ya kutumia mamilioni ya fedha za umma.
Kuhusu wanachama wa CCM ambao majina yao yamekatwa na NEC, Dk. Slaa
alisema milango iko wazi CHADEMA kwa wale wasio mafisadi kujiunga ili
kukielekeza chama hicho kushika dola mwaka 2015.
Alisema CHADEMA ni chama makini huenda kuliko vyama vingine, hivyo
hakiwezi kupokea wanachama kutoka CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi,
vinginevyo kitafunga milango na mapazia yake.
“Unajua, kuna watu wanaojulikana kwa ufisadi. Pia wapo wasafi
wanaoomba kujiunga na CHADEMA, hivyo watu safi hawana tatizo kujiunga na
CHADEMA kwa ajili ya kuunganisha nguvu kwenda kuongoza dola mwaka
2015,” alisema Dk. Slaa.
No comments:
Post a Comment