Katika hali ya kushangaza iliyotokea katika uchaguzi wa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) unaoendelea wilaya mbalimbali nchini, jana bundi wawili waliingia kwenye ukumbi wa mkutano mjini hapa.
Bundi hao nusura waangukie juu ya meza
waliyokuwa wamekaa Mbunge wa Jimbo la Kahama James Lembeli na Mwenyekiti
wa CCM Mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja.
Kitendo cha bundi hao kimetafsiriwa na
baadhi ya watu kuwa ni cha kishirikina. Hata hivyo, katika imani za
kiafrika, bundi anapoonekana maeneo ya nyumbani kwako au kulia juu ya
paa la nyumba yako, hiyo kitafsiri ni dalili mbaya sana ya mikosi
itakayokuandama baada ya hapo.
Imeelezwa kuwa vitendo vya kishirikina bado vimeshamiri kwa baadhi ya watu wanaowania kupata uongozi.
Hali hiyo ilizua mtafaruku mkubwa ndani ya
ukumbi wa mkutano hasa kwa wagombea wa nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM
wilayani hapa ambao walionekana kuwa na wasiwasi.
“Ni ajabu kweli bundi kuingia katika
ukumbi huku kukiwa na kelele kubwa na kutaka kuanguka katika meza za
viongozi, kitendo hicho ni cha kushitua sana,” alisema, Diwani wa kata
cha Chambo, Damas Joseph.
Alisema kuwa mambo hayo yanayohusiana na
imani za kishirikina katika chaguzi za CCM, hivyo ni muhimu yakakemewa
na chama kwani viongozi wanapaswa kuchaguliwa kwa haki kupitia kura
zinazopigwa na wajumbe.
Hata hivyo, alisema hadi sasa hakuna
malalamiko yoyote yaliyojitokeza wakati uchaguzi huo ukiendelea na
kuongeza miujiza hiyo iliyojitokeza ndio iliyoshtua wajumbe.
Mwanachama mwingine wa CCM kata ya Ukune,
Deo Ndilima, alisema kuwa kwa sasa bado vitendo vya kishirikina
havijaisha na kuongeza kuwa hali hiyo ni ya hatari hasa katika uchaguzi
na inasababisha chama kupata viongozi wasiofaa.
No comments:
Post a Comment