ASKARI polisi waliokuwa wamesheheni silaha jana waliweka ulinzi mkali
katika misikiti mikubwa ya jijini Dar es Salaam, wengine wakilazimika
kuyazingira makazi ya Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Shaaban Simba.
Mbali na kulinda maeneo hayo, askari hao pia walilazimika kuweka
ulinzi mkali katika ofisi za Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), wakiwa
tayari kukabiliana na kundi la Waislamu wenye msimamo mkali, ambao juzi
walitishia kufanya maandamano makubwa kwenda kuwang’oa madarakani,
Mufti Simba, pamoja na Katibu Mtendaji wa NECTA, Joyce Ndalichako, na
wasaidizi wake.
Ulinzi mkali pia uliimarishwa katika ubalozi wa Marekani, ambako
tofauti na sababu za kuvamia makazi ya Mufti na ofisi za Baraza la
Mitihani, kundi hilo lilipanga kuandamana kupinga hatua ya raia mmoja wa
nchi hiyo, kutoa filamu inayodaiwa kumkashifu Mtume Mohammed (SAW).
Magari mengi ya polisi yaliyokuwa na askari wa jeshi hilo, wakiwemo
wale wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) yalionekana katika misikiti
karibu yote mikubwa.
Magari hayo yalikuwa ni pamoja na yale ya maji ya kuwasha; pia
kulikuwa na polisi wa kikosi cha mbwa na wale waliokuwa wamevalia mavazi
ya kawaida wakiwa wametanda kila eneo la misikiti yakiwemo pia makao
makuu ya Bakwata, ambapo pia kuna msikiti mkubwa.
Katika msikiti wa Mtambani, magari mawili ya FFU yalikuwa yamesimama
hatua kadhaa kutoka ulipo msikiti huo, huku askari wake wakionekana kuwa
tayari kukabiliana na hali yoyote ya hatari.
Idadi kubwa ya waumini waliokuwa ndani ya msikiti huo waliendelea
kubaki ndani hata baada ya kumalizika kwa sala ya Ijumaa, ambapo mmoja
wa watu wanaoaminika kuwa kiongozi wa kundi hilo akisisitiza kuondolewa
kwa Mufti Simba na watu wake sambamba na NECTA na ubalozi wa Marekani.
Hata hivyo, baada ya muda wengi wao waliondoka kwa utaratibu bila
kufanya fujo wala kuandamana, huku kukiwa na madai kwamba watatimiza
azma ya kufanya maandamano ya kumwondoa Mufti Madarakani muda wowote.
“Kuuondoa utawala wa Bakwata kuko palepale, Waislamu tushikamane hilo
Jeshi la Polisi iko siku nalo litajua nini tunachokifanya!” alisikika
msemaji huyo akiwahimiza Waislamu katika msikiti huo.
Katika eneo la ubalozi wa Marekani Tanzania Daima lilishuhudia askari
wa Jeshi la Polisi likiwa limeweka doria hatua kadhaa kutoka katika
lango la ubalozi huo, huku wale wanaolinda ubalozi huo wakionekana kuwa
makini zaidi.
No comments:
Post a Comment