HATIMAYE Panga la Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais
Jakaya Kikwete, limewashukia vigogo wa chama hicho na kuwatupa nje ya
kinyang’anyiro cha kuwania nafasi za uongozi wa jumuiya za chama na
ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC).
Wakati panga hilo likiwashukia baadhi ya vigogo, Rais Kikwete ametoa
kauli nzito ya kutaka wagombea waliopata kutoa kauli za vitisho dhidi ya
chama hicho kufanya kile walichokusudia kukifanya.
Kikwete katika kauli yake hiyo alionekana waziwazi kukerwa na kauli za
‘patachimbika’ au zile za kutishia kujitoa na kujiunga na vyama vya
upinzani.
Akizungumza kwa ukali, Kikwete ambaye juzi alitamba akisema CCM
haitakufa kama inavyotabiriwa na baadhi ya watu, alihitimisha kauli yake
kwa kusema watu wenye kauli za namna hiyo walikuwa hawafai kuendelea
kuwa wanachama wa chama hicho.
Panga la Rais Kikwete limewaangukia wagombea wenye nyadhifa zaidi ya
moja serikalini na ndani ya chama pamoja na baadhi ya wabunge.
Wengine waliokatwa na vikao hivyo vya juu vya CCM vilivyomalizika jana
mjini Dodoma, ni wagombea waliokuwa wakiibua malumbano na wakati
mwingine kuikosoa CCM hadharani, makada waliojipambanua kama wapiganaji
na wapambanaji wa ufisadi na baadhi ya wabunge walioweka saini zao
bungeni kuunga mkono hoja ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe ya
kutaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ajiuzulu.
Habari kutoka ndani ya NEC, ziliwataja walioenguliwa kuwa ni pamoja na
Mbunge wa Nzega, Dk. Hamisi Kigwangalla na Mjumbe wa Baraza Kuu la
Vijana la CCM Taifa (UVCCM), Hussein Bashe.
Bashe na Kigwangalla ambao wamekuwa katika mvutano mkubwa wa kusaka
madaraka ndani ya chama, majina yao yalipendekezwa kukatwa kuwania
nafasi hiyo kuanzia kwenye sekretarieti, Kamati ya Maadili na Kamati Kuu
kabla ya kuthibitishwa na NEC.
Makada hao wamekuwa kwenye mvutano wa kisiasa uliodumu toka mwaka 2010
wakati wa uchaguzi mkuu ambapo Bashe alienguliwa kuwania ubunge, Jimbo
la Nzega na nafasi yake kuchukuliwa na Dk. Kigwangalla aliyeshika nafasi
ya tatu. Nafasi ya pili ilichukuliwa na mbunge wa zamani wa jimbo hilo,
Lucas Selelii.
Mbali ya hao, panga hilo limemkata Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.
Mgeja na Lembeli nao wamekuwa katika mvutano mkubwa ndani na nje ya
chama. Uhasama wao unachochewa na kambi mbili kubwa zenye uhasama
mkubwa.
Wengine waliokatwa ni Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina na Mbunge wa Ludewa, Deo Filukunjombe.
Wabunge hao ni miongoni mwa waliotia saini kutaka Waziri Mkuu Pinda
ang’oke. Duru za siasa zinasema kuwa msimamo wa wabunge hao kuhusu
Pinda, ndio ulisababisha wakatwe kuwania NEC.
No comments:
Post a Comment