Friday, September 14, 2012

IFAHAMU FILAMU INAYOTIKISA DUNIA YA KIISLAM KWA SASA

Taarifa mpya zimeanza kuibuka kuhusu chanzo cha filamu inayodhihaki dini ya kiisilamu na ambayo ndiyo chanzo cha machafuko nchini Misri na Libya na katika nchi zingine za kiisilamu.
Filamu hiyo iliyotengenezwa nchini Marekani, ilitolewa kwa mara ya kwanza katika ukumbi mmoja mjini Hollywood mwishoni mwa mwezi Juni.

Maandamano Tunisia
 Lakini ni baadhi ya picha za video za filamu hiyo zilizotolewa katika mtandao wa kijamii wa YouTube,zilizokuwa zimetafsiriwa kwa lugha ya kiarabu zilichochea maandamano yanayoshuhidiwa katika nchi za kiisilamu.
Filamu hiyo kwa jina - Innocence of Muslims - mwanzo ilitolewa kwenye mtandao tarehe mosi mwezi Julai ikiwa katika lugha ya kiingereza. Filamu hiyo iliwekwa kwa mtandao na mtu aliyetumia jina la "sambacile."
Kiwango cha utengezaji wa filamu hiyo ni duni sana, waigizjai wake hawana taaluma yoyote ya uigizaji pamoja na kuwa hadithi yake hata haieleweki.
Matamshi ambayo yanakejeli sana uisilamu na Mtume Muhammad, yalijitokeza zaidi katika muziki uliotumiwa kwenye filamu hiyo wala sio yale yaliyotamukwa na waigizaji.
Mmoja wa waigizaji walioigiza katika filamu hiyo alisema kuwa hakuwa na habari kuwa filamu hiyo ingetumika katika propaganda dhidi ya uisilamu na hivyo akailaani.
Cindy Lee Garcia,kutoka Bakersfield California,alinukuliwa katika taarifa kwenye mtandao wa Gawker akisema kuwa alikuwa na jukumu ndogo sana katika filamu hiyo ambayo aliambiwa ingeitwa -Desert Warriors- na kamba mada yake kuu ilikuwa tu maisha nchini Misri miaka 2,000 iliyopita.
Alitishia kumshtaki mtengezaji mkuu wa filamu hiyo kwa namna waigizaji walivyowakilishwa katika filamu hiyo.
Maswali yanayohojiwa.

Ghadhabu za waisilamu
Kimsingi filamu kwa jina -The Innocence of Bin Laden- ilionyeshwa katika ukumbi mdogo mjini Hollywood tarehe 30 mwezi Juni mwaka huu.
Mtu mmoja aliyeitizama filamu hiyo na ambaye hakutaka kutajwa,alisema kuwa ilikuwa ya saa moja na kwamba ilikuwa filamu duni sana ikizingatiwa utengezaji wake na kuwa ni watu wachache tu waliweza kuitizama.
Alisema kuwa mtu aliyefanya maandalizi ya kutizamwa kwa filamu hiyo ni raia wa Misri anayeishi nchini Marekani na ambaye alipewa ulinzi na watu wawili usiku huo.
Mwanaume mmoja kwa jina Sam Bacile, anayesema kuwa yeye ndiye aliyetunga filamu hiyo na hata kuitengeza, alizungumza na vyombo kadhaa vya habari na kutoa matamshi ya kuidhihaki dini ya kiisilamu wakati akiunga mkono filamu hiyo.
Alidai kuwa ana umri wa miaka 52 au 56, kulingana na vyombo kadhaa vya habari na kusema kuwa yeye ni Myahudi mzaliwa wa Israel ambaye alichangisha mamilioni ya dola kutoka kwa wahisani Wayahudi ili kutengeza filamu hiyo.
Lakini kabla ya wiki jana, mtu huyo hakujulikana hata kidogo kwenye mtandao, isipokuwa kwa jila alilotumia kuiweka filamu hiyo kwenye mtandao wa kijamii wa YouTube .
Maswali yameanza kuulizwa kuhusu ukweli wa jina la mtu huyo ,Sam Bacile, ikiwa ndiye kweli au anawahadaa tu watu.
Mmarekani mmoja mwenye siasa kali kwa jina Steve Klein, anayehusishwa na makundi yanayopinga uisilamu mjini Carlifonia, alitoa hamasisho kubwa kuhusu filamu hiyo, ingawa alisema hajui nani aliyeitengeza.
Hata hivyo alitoa taarifa zilizogongana wakati akihojiwa na vyombo kadhaa vya habari kuhusu misimamo yake
mikali na kisha kukubali kuwa hakuna mtu kwa jina la Sam Bacile, ni jina tu lililotolewa kuwahadaa watu.
Kasisi Terry Jones kutoka mjini Florida, ambaye vitendo vyake vya kupinga uisilamu vikiwemo kuteketeza kitabu kitakatifu cha Quran, alisema kuwa aliwasiliana na bwana Bacile kuhusu kuhamasisha watu juu ya filamu hiyo lakini hakuwahi kukutana naye ana kwa ana na wala hawezi hata kumtambua.
Uhusiano wa Kikopti?
Jina lengine lililoonekana kuhusishwa na filamu hiyo ni lile la - Morris Sadek - raia mmoja mzaliwa wa Misri ingawa anaishi Marekani kutoka kwa vuguvugu la kikopti ambalo linapinga uisilamu.
Hatua yake ya kuhamasisha kuhusu filamu hiyo ilizua maswali mengi juu ya uhusiano wa filamu yenyewe na makundi ya wakristo wa kikopti.
Idadi ya wakristo wakopti nchini Misri ni kubwa kiasi ingawa wao ni wachache ikilinganishwa na wakristo wengine na kwamba watu wamezua maswali mengi kuhusu uhuru wao wa kidini katika utawala mpya wa Misri chini ya uongozi wa rais wa chama cha Muslim Brotherhood.
Shirika la habari la AP, ambalo lilimhoji kwa njia ya simu mtu anayedai kuwa ndiye Sam Bacile, na inasemekana alisema kuwa yeye ni mkristo mkopti na kwamba alihusika katika usimamizi wa shughuli za kuitengeza filamu hiyo.
Filamu hiyo ilionyeshwa kwa mara ya kwanza katika internet na nia hasa ya kuitengeza ingali kizungumkuti. Lakini hakuna dalili kuonyesha kuwa inahusishwa na mtengezaji filamu wa Israel kama ilivyoripotiwa awali hata na BBC.
Kilichowauma wengi sana, ni filamu hiyo kutafsiriwa katika lugha ya kiarabu na kuonyeshwa katika vituo vya televisheni vya kiarabu. Hii ndiyo hatua iliyochochea maandamano makubwa katika nchi za kiarabu.

No comments:

Post a Comment