Saturday, September 8, 2012

ASEMAVYO BABA MZAZI WA DK.ULIMBOKA KUHUSU ALIPO MWANAE.

BAADA ya kimya cha muda mrefu, baba mzazi wa kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk Stephen Ulimboka, amekubali kuzungumzia sakata la mwanaye kutekwa, kuteswa, kutibiwa na hatimaye kurejea nchini akisema kwamba kupona kwake ni neema za Mungu, huku akiishutumu Serikali kuwa imewatelekeza Watanzania.
Hii ni mara ya kwanza kwa baba huyo, Ulimboka Mwaitenda kuzungumza tangu mwanaye alipotekwa, kuteswa na baadaye kutupwa katika Msitu wa Pande, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
“Naishangaa Serikali hii ambayo wananchi wanapigwa na kuuawa bila makosa. Nakumbuka kiongozi aliyeipenda Tanzania ni mmoja na ameshatangulia mbele za haki,” alisema akimaanisha Baba wa taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Mwaitenda alitoa kauli hiyo jana baada gazeti hili kumtafuta ili azungumzie habari zilizoenea nchini kwamba mwanaye, amepata kazi nje ya nchi.
Kuhusu madai hayo, Mwaitenda alikanusha akisema kuwa mtoto wake hawezi kwenda nje ya nchi bila yeye kufahamu... “Pengine ana mipango hiyo, lakini mimi sijui wala sijasikia, lakini atakwenda nje ya nchi kufanya nini? Hizi habari hizo ndiyo nazisikia kwako kwa mara ya kwanza eti Ulimboka anataka kwenda nje ya nchi? Akafanye nini alichokosa hapa Tanzania!”
Wakati mwandishi akiingia nyumbani kwa Mwaitenda, Ubungo Kibangu, Dar es Salaam, alipishana na Dk Ulimboka akiwa kwenye gari na wenzake, wanne. Hata hivyo, hakufanikiwa kuzungumza naye.
Kuhusu tukio la kutekwa, kuteswa na kutupwa katika Msitu wa Pande, Mwaitenda alisema: “Mpaka sasa, tumeiona kazi ya Mungu, ile ni neema ya Mungu kwa sababu wewe uliona wapi mtu akapigwa namna ile halafu akapona kama si kwa neema tu.”
Madai Dk Ulimboka kutoweka
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Namala Mkopi ambaye alikuwa karibu na Dk Ulimboka wakati wa mgomo wa madaktari nchini, alisema tangu waonane aliporejea nchini kutoka Afrika Kusini, hajawasiliana tena.
“Hatujawasiliana naye,” alisema Dk Mkopi na kusema kulingana na ukubwa wa tatizo lililompata, hakuwa na mpango wa kumsumbua, bali kumwacha apumzike hadi atakapokuwa amejisikia mwenyewe kurejea kazini.
Aliyekuwa kiongozi wa jopo la madaktari waliomhudumia, Profesa Joseph Kahamba alisema, hajawahi kuonana wala kuwasiliana na Dk Ulimboka tangu alipopelekwa Afrika Kusini, Juni mwaka huu.

No comments:

Post a Comment