Mwanasiasa tatanishi nchini Afrika Kusini Julius Malema amezuiwa kuwahutubia wafanyakazi wa migodini wanaogoma katika mgodi wa Marikana.
Migomo ya wachimba migodi ambayo inakumba nchi hiyo tayari imeathiri uzalishaji wa madini ya dhahabu na Platinum katika nchi hiyo ambayo ina utajiri mkubwa wa maliasili.
Rais Jacob Zuma amesema kuwa hatua ya wachimba migodi imesababisha hasara ya karibu dola milioni 548 kwa sekta ya madini.
Akiongea kabla ya kongamano la vyama vya wafanyakazi nchini humo, (Cosatu) Zuma alisema kuwa migomo ya mwaka huu imekosesha hazina ya fedha dola milioni 388.
Wiki jana serikali ilisema kuwa itachukua hatua za dharura dhidi ya wale wanaochochea fujo na hivyo kuisababishia sekta ya madini mamilioni ya hasara.
Baada ya kutofautiana na polisi waliokuwa wanalinda uwanja huo, Malema alisindikizwa na kikosi maalum cha polisi hadi mbali sana na uwanja huo. Magari mawili ya polisi yenye silaha yalifuata gari la Malema na juu angani kukawa na helikopta iliyokuwa inamfuata pia.
Ametoa wito wa maandamano ya kitaifa baada ya hapo awali, kusema kuwa shughuli za migodi lazima zitatizwe.
Malema amekosolewa na wengi ambao wanamuona kama mwenye njama ya kutumia masaibu ya wafanyakazi wa migodini kujinufaisha kisiasa hasa baada ya wachimba migodi 34 kuuawa na polisi wakati wa mgomo wao katika mgodi wa Marikana mwei jana.
No comments:
Post a Comment