mh.John Mnyika |
Mnyika pia amemtaka Rais Kikwete awaambie wakazi wa Ubungo kuhusiana na viwanda kadhaa vilivyo ndani ya jimbo lake, ambavyo vingekuwa chachu ya maendeleo ya wananchi, lakini vimefungwa.
Mbunge huyo alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kuzindua ofisi, pamoja na kuweka mawe ya misingi katika kata ya Mabibo ambapo alieleza kushangazwa kwake na kutotekelezwa kwa ahadi hewa zilizotolewa na kiongozi huyo wakati wa uchaguzi mkuu uliyopita.
Mnyika alivitaja baadhi ya viwanda hivyo vilivyobinafsishwa kuwa ni Ubungo Garments, Spinning Mill, Polysack Lmt, Tanzania Sewing Thread, Coastal Diaries, pamoja na kiwanda cha Zana za Kilimo (UFI).
“Tunamshinikiza Kikwete kama kiongozi wa nchi pamoja na Baraza la Mawaziri kurejesha viwanda vilivyobinafsishwa kiholela katika jimbo la Ubungo ili kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira linalowakabili Watanzania,” alisema Mnyika.
Katika hilo, alimtaka mwenyekiti wa baraza hilo ambaye ni Rais kutoa kauli ya matokeo ya maafikiano ya pamoja waliyoafikiana na mawaziri juu ya ajira hizo ili kuondoa utata uliopo baina ya wananchi na viongozi wao wa kada husika.
Alitanabaisha kuwa ili kukabiliana na tatizo la ajira katika jimbo hilo, manispaa ya Kinondoni imetenga fedha zaidi ya sh milioni 200 kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya kinamama pamoja na vijana.
Alitumia fursa hiyo kuitaka manispaa hiyo kutoa kipaumbile katika suala la ajira hasa kwa kuwafikia walengwa badala ya kuishia mikononi mwa wachache.
“Nawataka na ninyi wananchi mliojiunga katika vikundi mbalimbali vya kukopeshwa kufuatilia kwa makini fedha hizo ngazi husika, ila mkikwama tafadhali rudini kwangu kwa ripoti maalumu ili nifuatilie suala hilo ambalo ni muhimu kwetu,” alisema mbunge huyo.
Rais Kikwete ndiye mgombea aliyeongoza kwa kutoa ahadi nyingi wakati wa kampeni za uchaguzi kuliko wagombea wengine wa nafasi ya urais kutoka vyama hasa vya CHADEMA na CUF.
No comments:
Post a Comment