MADAI ya utabiri wa kifo cha Chama cha Mapinduzi (CCM), yamemfikia
Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, ambaye amejigamba kuwa
wanaotabiri kifo hicho, watakufa wao kabla chama.
Rais Kikwete alitoa majigambo hayo jana wakati akifungua kikao cha
Kamati Kuu ya (CC) mjini hapa, kilichofanyika katika ukumbi wa makao
chama hicho.
Alisema kuwa kikao cha Kamati ya Maadili kilichomalizika jana saa 9
alfajiri kilikuwa na majina mengi ambayo yalitakiwa kupitiwa kwa umakini
zaidi ili kuweza kutenda haki kwa walioomba nafasi mbalimbali za
kugombea uongozi ndani ya CCM.
Rais alifafanua kuwa licha ya kuwepo kwa majina mengi ya wagombea
nafasi mbalimbali lakini kikao hicho kimeweza kufanya mabadiliko tofauti
na mapendekezo yaliyotoka mikoani.
“Tumefanya kazi kubwa sana katika kupitia majina ya waliopitishwa
kugombea nafasi ya Halmashauri Kuu (NEC) kutoka mikoani kwanza walikuwa
wengi na wasomi pia walikuwepo wengi.
“Hata kikao cha maadili tumepitia majina ya wagombea kwa umakini na
kufanya mabadiliko tofauti na mapendekezo ambayo yaliletwa kutoka
mikoani, tumejaribu kujihoji ni kwa nini huyu kapewa alama hii na huyu
kanyimwa alama hii,” alisema Kikwete.
Alisema kuwa Kamati ya Maadili ilikuwa ikipitia jina moja hadi
jingine, na yamefanyika mabadiliko ya mapendekezo ya wagombea kutoka
ngazi za mikoani.
“Kikao cha Kamati ya Maadili kilikuwa kikubwa zaidi na chenye kuhitaji
umakini mkubwa na ndiyo maana tulimaliza saa 9 alfajiri, lengo lilikuwa
ni kupitia majina kwa usahihi lakini kikao hiki natarajia kitakuwa
chepesi na kitaisha mapema saa 6 usiku, wajumbe msiwe na wasiwasi,”
alisema Kikwete.
Kauli ya Rais Kikwete kuwa Kamati ya Maadili
imeyapitia majina yote moja baada ya jingine na kufanya mabadiliko
tofauti na mapendekezo yaliyotoka mikoani, inaelezwa kuanza kuwaweka
matumbo moto baadhi ya vigogo.
Tanzania Daima imedokezwa kuwa kumekuwa na shinikizo kubwa ndani ya
chama la kumtaka Rais Kikwete kuwatosa baadhi ya vigogo kwa kukata
majina yao kutokana na tuhuma mbalimbali zinazowakabili ili wasigombee.
Majina yanayotajwa kufikishwa kwa Rais ili yapigwe panga ni pamoja na
Edward Lowassa anayewania ujumbe wa NEC Wilaya ya Monduli na Andrew
Chenge ambaye amepita bila kupingwa huko Bariadi.
Kwa upande wa vijana wanatajwa ni Makamu Mwenyekiti wa sasa wa UVCCM,
Beno Malisa, Hussein Bashe, Anthony Mavunde, Jaml Kassim, Salum Salehe
na Fred Lowassa ambao inasemekana wanatumiwa kama mawakala kumwaga fedha
za kuhakikisha maslahi kambi ya kigogo mmoja inaimarika kuelekea
uchaguzi mkuu 2015.
No comments:
Post a Comment