WAKATI Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), ikitangaza chaguzi ndogo za
madiwani katika kata 29 za Halmashauri 27 nchini utakaofanyika Oktoba
28, mwaka huu, viongozi wa vyama vya upinzani wamelalamika wakisema
imeshindwa kusimamia uchaguzi huru na wa haki.
Akizungumza katika
mkutano na viongozi wa vyama vya siasa, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji
Damian Lubuva amesema ratiba ya uchaguzi hiyo imeshatolewa na kwamba
tume hiyo imejiandaa vya kutosha kuhakikisha uchaguzi huo unafanikiwa.
“Tume
tayari imekwisha toa ratiba nzima ya chaguzi hizi kuanzia siku ya
kupiga kura. Tunatarajia vyama vya siasa vitakavyoshiriki chaguzi hizi
pamoja na wadau wengine watazingatia ratiba hii na kuifuata kwa makini
ili kuepusha usumbufu utakaoweza kujitokeza endapo ratiba itakiukwa,”
alisema Jaji Lubuva. Licha ya kutaja hatua ya wapiga kura
kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, Jaji Lubuva
alisema daftari litakalotumika ni lile la mwaka 2010 na kwamba daftari
hilo litarekebishwa kabla ya mwaka 2015. Kwa upande wake
Mkurugenzi mtendaji wa tume hiyo, Julius Malaba fomu za uteuzi wa
wagombea zimeanza kutolewa na wasimamizi wa uchaguzi kuanzia jana (juzi)
Septemba 19, 2012 na zitaendelea kutolewa hadi Oktoba 2, 2012 kuanzia
saa 1.30 asubuhi hadi 9.30 alasiri siku za kazi.
Malalamiko ya vyama vya siasa
Wakitoa
maoni hayo katika mkutano huo, viongozi wa vyama vya siasa waliikosoa
Tume hiyo wakisema imeshindwa kusimamia chaguzi nchini.
Mwenyekiti
wa Chama cha National League for Democracy, Dk Emmanuel Makaidi alisema
utendaji wa Tume hiyo ni mbovu ndiyo maana baada ya uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010 kumekuwa na kesi nyingi za kupinga matokeo,
“Kama kuna
tume inayofanya madudu basi ndiyo hii, ilifanya hivyo kwenye uchaguzi
mkuu wa mwaka 2010 ndiyo maana kuna kesi 47 za kupinga matokeo,” alisema
Dk Makaidi na kuongeza:
“Tume ile ilishiriki katika kuchakachua
uchaguzi… sioni ajabu Mwenyekiti na mkurugenzi kuondolewa.. ikiendelea
hivi nchi itaingia vitani na Nec itawajibika,”
Naye Kaimu Katibu mkuu wa UDP, Isaac Cheyo alisema tume hiyo haina nguvu ya kusimamia sheria na maadili yaliyopo,
“Umesema
maadili yanakataza vyama kutoa lugha chafu, kama ikitokea mlalamikaji
aende kwenye kamati ya maadili inayoongozwa na Katibu tawala wa mkoa na
wilaya na katibu tarafa. Hawa hawana mamlaka ya kushughulikia,” alisema
Cheyo.
Aliongeza kuwa licha ya daftari la kudumu la wapiga kura kupitiwa, mchakato wake haukuwashirikisha wananchi.
“Ni
Daftari bovu, mwaka 2009, Serikali ilifanya mabadiliko ya vijiji na
kata. Ilipofika wakati wa uchaguzi mtu amejiandikishia kata Fulani,
anaambi wa jina liko kata nyingine…” alisema.
Naye Mkurugenzi wa
uchaguzi wa Chadema, Msafiri Mtemelwa alisema tatizo la Nec ni kutokuwa
na mtandao nchi nzima badala yake inatumia maofisa wa Serikali.Aliongeza
kuwa mfumo mzima wa uchaguzi unalenga kukinufaisha CCM na kuvikandamiza
vyama vya upinzani,“Tatizo sijui CCM wanataka watawale milele…
kuna kata 12 nchini hazijafanya uchaguzi mwaka mzima. CCM wanaangalia
kama watashinda, wakiona wanashindwa wanamwambia Waziri wa Tamisemi
aahirishe uchaguzi…” alidai Mtemelwa.
Naye mwakilishi kutoka
NCCR Mageuzi, Faustine Sungura aliitaka Tume hiyo kuwalipa mawakala wa
vyama vya siasa kama vile inavyowaapisha kutunza siri zake,“Ki uhalisia
mimi mgombea sina wakala, kwa sababu unamwapisha ili atunze siri za
tume, mmeshamchukua. Basi muwalipe,” alisema Sungura.
Akijibu
maoni hayo, Jaji Lubuva alisema tangu ameingia katika tume hiyo amekuwa
na nia ya kuona tume hiyo inakuwa huru lakini bado Serikali
haijatekeleza maombi yake. “Tangu nilipoapishwa kushika nafasi
hii, nia yangu ni kutatua kasoro hizo.. lakini hiyo ni kazi ya Serikali,
kwa mfano hilo la kuwa na mtandao nchi nzima wanasema leteni bajeti,”
alisema Jaji Lubuva na kuongeza:
“Nilipokwenda kujitambulisha
Zanzibar, Rais aliuliza, mbona hamna ofisi?..Hayo ya uhuru wa tume
tumeshayazungumza sana, lakini wakati wa kutangaza mshindi, hawa wajumbe
wote wanahusika siyo mtu mmoja.”
No comments:
Post a Comment