WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, jana alijikuta katika wakati mgumu baada
ya kushindwa kuhutubia maelfu ya wakazi wa Wilaya ya Nyamagana,
jijini Mwanza kwa muda kutokana na wananchi wengi kumzomea.
Kiongozi huyo alikumbana na kisanga hicho cha aina yake akiwa na
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza, Clement Mabina pamoja na Mkuu wa Mkoa
huo, Mhandisi Evarist Welle Ndikilo.
Pinda na viongozi hao, walikumbana na zomeazomea hiyo kwenye mkutano
wa hadhara uliofanyika viwanja vya Sahara jijini hapa, ikiwa
ni hitimisho la ziara ya Waziri Mkuu huyo ya siku saba mkoani Mwanza.
Chanzo cha Pinda na viongozi hao kuzomewa mkutanoni hapo, ilitokana na
kile kilichoonekana kuwepo kwa kero nyingi zilizodaiwa kushindwa
kupatiwa ufumbuzi na Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete.
Kitendo hicho cha wananchi kilimlazimisha Pinda kushindwa kuhutubia kwa muda, huku akionekana kujawa jazba.
Sababu nyingine ya wananchi kuzomea, ni hatua ya Pinda kuwaambia
wananchi hao watoke mjini waende vijijini wakalime waachane na mambo ya
upinzani wa kisiasa.
Pinda alitoa kauli hiyo baada ya kundi la vijana mkutanoni hapo
kuonesha alama ya V, bendera ya CHADEMA na nyimbo za Peoples, Power.
Kwa mazingira hayo, askari wa polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia
(FFU), waliokuwa na silaha nzito za kivita aina ya SMG, mabomu na
marungu waliokuwepo mkutanoni hapo, walianza kuwatishia kuwapiga
wananchi hao kwa lengo la kumlinda kiongozi huyo.
Baada ya kuzidi zomeazomea hiyo, Waziri Mkuu, Pinda alilazimika
kumuita mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (CHADEMA), aliyekuwa meza
kuu, kisha kusema: "Nyamazeni basi!. Wenje...hii ndiyo serikali ya siku
chache zijazo. Kwa namna hii naona hamuwezi, maana itakuwa ni vurugu
asubuhi hadi jioni". Akazomewa kisha wakaimba hatutaki CCM, hatutaki
CCM. .
Baada ya kuona hivyo, Pinda akacheka na kusema: "Hahahaaaaa, hata
mkiimba peoples power, CCM ndiyo inayowaongoza". Akazomewa tena kisha
Pinda akashindwa kuendelea kuzungumza jukwaani.
No comments:
Post a Comment