Saturday, September 15, 2012

BAADHI YA MABADILIKO LIGI KUU TANZANIA BARA

KAMATI ya Mashindano ya Shirikisho la Soka (TFF), imerekebisha kanuni za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ambapo sasa mechi zitakazoahirishwa kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo mvua, zitarudiwa siku inayofuata kwa muda uliobaki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Mashindano wa TFF, Saad Kawemba, alisema kuwa marekebisho hayo yamefanyika kutokana na malalamiko ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo.
Kawemba alisema kuwa awali ilikuwa ikitokea matatizo kwenye mechi kama ya mvua na mengineyo, mechi ilikuwa inaanza upya siku inayofuata, lakini sasa itakuwa tofauti na hivyo.
“Kwa sasa, mechi zote zitakazokuwa zikiahirishwa kwa sababu mbalimbali, zitarudiwa siku inayofuata kwa muda ule uliokuwa umebaki tu kabla ya kumalizika kwa pambano, huku mabao pamoja na kadi, zikiwa ni zilezile,” alisema Kawemba.
Alisema kuwa mbali na kanuni hiyo, kadhalika mdhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, sasa atakaa kwenye mabega si kifuani kama ilivyokuwa awali na mdhamini wa klabu ndiye atakayekaa kifuani.
Kawemba alisema mabadiliko hayo yamekuja baada ya klabu kukaa na kuomba mdhamini wao akae mbele, huku mdhamini wa ligi akiwa kwenye bega, ambapo ombi hilo limekubaliwa.
Aidha alisema kuwa iwapo kikosi cha timu ya taifa kitakuwa na mechi yoyote ya kimataifa, Ligi Kuu kwa sasa itasimama ili kuwapa nafasi wachezaji kutumikia kikosi chao cha taifa.
“Ilivyokuwa mwanzo ni kwamba wachezaji zaidi ya watano ambao ni tegemeo wakiwa kwenye timu ya taifa, mechi za Ligi Kuu ziliendelea, lakini kwa sasa mechi hizo zitakuwa zinasimama,” alisema Kawemba.
Aliongeza kuwa wachezaji wa kigeni wanaotumika Ligi Kuu, wanatakiwa wasizidi watano, ambapo kanuni hiyo imefuatwa na klabu nyingi zinazoshiriki michuano hiyo inayoanza leo.
Alisema kuwa mwanzoni mwa mwaka huu, ilikuwa ni mwisho wachezaji watano, ila klabu ziliomba, ambapo ombi lao limekubaliwa mwisho mwaka 2014/2015, ili kutoa nafasi kwa wazawa kuonyesha viwango vyao.
Kawemba alitoa mfano, mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi, na kiungo Haruna Niyozima wa Yanga, kuwa ndiyo pekee waliofanya vema kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara, ukiacha wachezaji wote wa kigeni waliosajiliwa katika klabu mbalimbali.

No comments:

Post a Comment