ENTERTAIMENT




WANAMUZIKI maarufu Afrika, Papa Wemba wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, 2 Face Idibia wa Nigeria, Ambwene Yessaya 'AY' wa Tanzania na Daddy Owen wa Kenya watatumbuiza kesho katika fainali za michuano ya soka ya vijana ya Airtel Rising Stars zitakazofanyika kwenye Uwanja wa Nyayo, Nairobi.Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na waandaaji wa michuano hiyo, wanamuziki hao wataanza kutoa burudani kuanzia mchana, ambapo kila msanii atatumbuiza nyimbo zake maarufu zilizompatia umaarufu ndani na nje ya nchi yake. Baadhi ya nyimbo hizo ni ‘African Queen’, na ‘If love is a crime’ za 2 Face Idibia, ‘Show me the way’, ya Papa Wemba na ‘Bed n Breakfast‘, ‘Goodlook’ ‘Freeze’ za Ay.   Michuano hiyo ya Airtel Rising Stars ilifunguliwa Jumatatu iliyopita na Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, ambapo imeshirikisha jumla timu 15 za Afrika na mechi ya kesho ya fainali itaonyeshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sports cha Afrika Kusini. Nchi zilizoshiriki ni wenyeji Kenya, Tanzania, Madagascar, Malawi, Ghana, Zambia, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Burkina Fasso, Chad, Congo Brazaville, Uganda, Niger, Nigeria na Sierra Leone.Katika hatua nyingine, habari zilizotufikia jana kutoka Nairobi ni kwamba timu ya Tanzania ilikuwa nyuma kwa mabao 2-1 dhidi ya Zambia katika mchezo wa mwisho uliokuwa ukichezwa kwenye uwanja Nyayo. Kama matokeo yatabaki hivyo, hiyo inaamanisha vijana wa Tanzania watakuwa wameaga mashindano hayo kwani mechi ya kwanza walifungwa bao 1-0 na Gabon kabla ya kutoka sare ya 1-1 na Burkina Fasso.