Mwanaharakati wa kisiasa nchini
Afrika Kusini Julius Malema, amewashauri wanajeshi wenye manung'uniko
kujipanga vyema na kupigania kazi zao.
Malema aliyatoa matamshi hayo kwa wanajeshi
wanaokabiliwa na makosa ya kinidhamu yaliyotokana na maandamano
waliyoyafanya mwaka 2009 wakidai mishahara mizuri na mazingira bora ya
kazi.
Bwana Malema ni mwanasiasa anayeibua mgawanyiko
hapa. Hivi maajuzi alifukuzwa kutoka chama cha ANC na kwa sasa
anafanyiwa uchunguzi kuhusiana na kashfa ya ufisadi.
Lakini hajaondoka ANC kimya kimya. Badala yake
ametumia mauaji ya hivi maajuzi katika mgodi wa Marikana kuanzisha
kampeni kali dhidi ya mabepari nchini Afrika Kusini na kutaka yafanyike
mapinduzi ya kiuchumi.
Wengi wanamshutumu kwa kuhusika na ubinafsi
mbaya wa kisiasa, lakini malema anapokea uungwaji mkubwa kutoka kwa
jamii za watu maskini na kimya cha serikali ni ishara tosha kuwa
imeshindwa kukabiliana naye.
Manung'uniko ya wanajeshi ni fursa nyingine kwa Malema kuonyesha ubabe wake na hali ni tete nchini Afrika Kusini.
Hofu iliyopo ni kwamba migomo huenda ikaenea
zaidi na kwamba serikali kwa sasa inazingirwa na migogoro ya ndani huku
baadhi ya mirengo serikalini ikipanga njama ya kumtimua madarakani rais
Jacob Zuma.
No comments:
Post a Comment