Monday, September 10, 2012

OKWI ALETA KICHEKO NA MATUMAINI MSIMBAZI

KIKOSI cha mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Simba, kimezidi kuimarika baada ya mshambuliaji wake wa kimataifa, Emmanuel Okwi, kurejea jana na leo anatarajiwa kuungana na wenzake katika mazoezi yanayoendelea kwenye viwanja vya TCC Chang’ombe.
Okwi alikuwa akiitumikia timu yake ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ ambayo juzi ilicheza mechi ya kuwania nafasi 15 za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani na kufungwa bao 1-0 anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba watakoshuka katika dimba la Taifa jijini Dar es Salaam kesho kukipiga na Azam FC katika mchezo maalumu wa kuwania Ngao ya Hisani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ofisa habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema kwamba ujio wa Okwi umeongeza makali ya timu yao katika mchezo wao na Azam kesho pamoja na Ligi Kuu kwa ujumla inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Septemba 15.
Alisema kikosi cha Simba kipo katika hali nzuri kikiendelea na maandalizi yake ya mchezo huo huku pia mshambuaji wake mwingine wa kimataifa, Mzambia Felix Sunzu, aliyekwenda kumzika dada yake Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) akitarajiwa kuwasili leo.Katika hatua nyingine, Kamwaga alisema licha ya kupoteza mchezo wao wa mwisho wa kirafiki dhidi ya Sofapaka ya Kenya kwa kufungwa mabao 3-0, hasira za kipigo hicho watazimalizia kesho kwa Azam.
Alisema kipigo cha Sofapaka kimemfanya kocha Mkuu wa timu hiyo, Mserbia Milovan Cirkovic, kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza hususani katika safu ya ulinzi iliyosababisha wapinzani kupenya.

No comments:

Post a Comment