Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
kimeiponda tume ya Dk Nchimbi kikieleza kuwa imeundwa ili kurudisha
uhusiano kati ya Polisi na waandishi wa habari na si kutafuta chanzo cha
tatizo.
Juzi, Dk Nchimbi alitangaza kamati ya kuchunguza mauaji
hayo inayoongozwa na Jaji Mstaafu, Steven Ihema na wajumbe, Mwakilishi
wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Theophil Makunga, Mwakilishi wa
Baraza la Habari Tanzania (MCT), Pili Mtambalike, Mtaalamu wa milipuko
kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kanali Wema Wapo na Naibu
Kamishna wa Polisi (DCP), Isaya Mngulu.
Mkurugenzi wa Sheria,
Katiba na Haki za Binadamu wa Chadema, Tundu Lissu alisema Dar es Salaam
jana kwamba: “Hii si tume ya kuchunguza mauaji, bali ina lengo la
kurudisha uhusiano mzuri kati ya Jeshi la Polisi na waandishi wa habari
ili kuwasahaulisha wananchi kwa sababu imeundwa na waziri ambaye naye
anatakiwa kuhojiwa.” “Tunamwomba Rais Jakaya Kikwete ateue tume kama
anavyoelekezwa na Sheria ya Tume za Uchunguzi ya mwaka 1992, ambayo
inaruhusu kumhoji yeyote kasoro yeye Rais.”
Lissu alisema Rais
Kikwete angeunda tume hiyo na Waziri Nchimbi na IGP Said Mwema
wanatakiwa kujiuzulu ili kupisha uchunguzi akidai kwamba kuna uwezekano
mkubwa kwamba walitoa amri ya mauaji hayo.
“Dk Nchimbi anatakiwa
kumuiga Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi ambaye alijiuzulu akiwa
Waziri wa Mambo ya Ndani baada ya kutokea mauaji, akijiuzulu
atajijengea heshima tofauti na sasa kwani wananchi wamesikitishwa na
mauaji hayo,” alisema Lissu.
Mwanasheria wa Chadema, Mabere
Marando alidai kwamba kuna mkakati uliowekwa na Serikali wa
kukidhoofisha Chadema baada ya kuonekana kwamba ni tishio kwa CCM.
Mbali
na Chadema, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), pia
limesema halina imani na kamati hiyo likisema imekuwa kawaida kwa
Serikali kuunda tume ambazo hazileti ripoti kwa wananchi.
“Tume
zimekuwa zikiundwa bila faida yoyote, huku zikipewa muda kuchunguza
yaliyotokea lakini matokeo yake huwa hakuna ripoti wanayorudisha,”
alisema Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Hezron Kaaya.
Kaaya alisema
tume zimekuwa zikiundwa na kuigharimu Serikali fedha nyingi za walipa
kodi, lakini ripoti zake zinaendelea kuwa siri.
Imeandikwa na Habiel Chidawali, Dodoma, Hamida Sharrif Morogoro, na Tumaini Msowoya, Iringa na
Lasteck Alfred na Juliana Malondo.
No comments:
Post a Comment