uchaguzi wa mameya wa wilaya mbili za Nyamagana
na Ilemela jijini Mwanza, unatarajiwa kufanyika leo huku mnyukano mkali
ukiwa katika halmashauri ya Nyamagana kutokana na CCM na CHADEMA kuwa
na idadi sawa ya viti vya madiwani na hivyo kutegemea kura za CUF ziamue
mshindi.
Katika Halmashauri ya Ilemela, CHADEMA ina uhakika wa asilimia mia
moja kutokana na kuwa na madiwani wengi kuzidi wenzao wa CCM huku
mikakati yao ikilenga kuwashirikisha CUF ili waitwae pia Nyamagana.
Uchaguzi huo unafanyika baada ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza
kugawanywa na hivyo kuzaa halmashauri hizo mbili. Lakini pia Halmashauri
ya Jiji la Mwanza kwa sasa muda kadhaa haikuwa na Meya baada ya Baraza
la Madiwani kumvua wadhifa huo, Jackson Manyerere (CHADEMA).
Baada ya meya kuenguliwa, kulizuka mtafaruku ndani ya CHADEMA jijini
hapa ambao ulisababisha madiwani wawili kutimuliwa uanachama kwa kile
kilichodaiwa ni usaliti wa kuanzisha hoja ya kumtosa kiongozi huyo.
Hivyo kutokana na CHADEMA kutokuwa na madiwani hao, inaingia kwenye
uchaguzi wa leo ikiwa na madiwani sita na mbunge Ezekiel Wenje katika
wilaya ya Nyamagana wakati wenzao CCM wana madiwani saba na CUF wawili.
Kwa mnyukano huo ni dhahiri kuwa CHADEMA na CCM watakuwa wamefungana
kwa kura na hivyo kuhitaji huruma ya madiwani wa CUF ili upande mmoja
uibuke kidedea.
Taarifa za uhakika kutoka jijini hapa ni kwamba CHADEMA wamefanya
mazungumzo ya kushirikiana na CUF kwa kuwaachia nafasi ya Naibu Meya
ambayo itagombewa na diwani wao wa kata ya Mirongo, Daud Mukama.
Kwa halmashauri ya Ilemela CHADEMA wana uhakika wa kuibuka kidedea
kutokana na kuwa na madiwani wanane na mbunge Highness Kiwia huku wenzao
wa CCM wakiwa na madiwani sita na CUF ina mbunge wa Viti Maalum, Mkiwa
Kimwanga.
Kamati za utendaji za CHADEMA katika wilaya hizo zimefanya vikao
tofauti kwa kushirikiana na kamati za madiwani na kukamilisha mchakato
wa kupata wagombea wao.
Kwa mujibu wa ofisa habari wa CHADEMA, Tumaini Makene, kamati ya
utendaji ya wilaya pamoja na madiwani wa Nyamagana walimteua aliyekuwa
Naibu Meya kabla, Diwani wa Kata ya Maina, Charles Chibara, kuwa mgombea
wa umeya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Kwa upande wa Ilemela, kikao cha kamati ya utendaji pamoja na madiwani
walimteua Diwani wa Kata ya Nyamanoro, Abubakar Kapera, kuwa mgombea wa
umeya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela.
Kikao hicho cha Ilemela, pia kilimteua Diwani wa Kirumba, Danny
Kahungu, kuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Meya halmashauri hiyo wakati
kamati ya utendaji ya Nyamagana imekubali kumwachia kugombea nafasi ya
Naibu Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Diwani wa Mirongo, Daudi
Mkama (CUF).
Wao CCM wamemteua Diwani ya Kata ya Mkolani, Stanslaus Mabula,
kugombea nafasi ya umeya katika halmashauri ya jiji la Mwanza huku
diwani wa kata ya Igogo, John Minja, akigombea unaibu meya na Ilemela
wagombea ni Renatus Kalunga na naibu wake Sarah Ng’hwanu.
No comments:
Post a Comment