Tuesday, September 11, 2012

MJUE RAIS MPYA WA SOMALIA-ALISOMA CHUO KIKUU SOMALIA

Rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud



 Viongozi wa kimataifa wakiwemo Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron, wamepongeza uchaguzi wa rais mpya wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud kama hatua muhimu kwa Somalia.
Bwana Cameron amempongeza Sheikh Mohamud kwa ushindi wake, na vile vile kumsifu rais anayeondoka Sheikh Sharif Sheikh Ahmed kwa uongozi wake.
Somalia imekuwa vitani kwa miongo miwili.
Akikubali kushindwa, rais anayeondoka, Ahmed Shariff, alisema kuwa huo ndio ulikuwa uchaguzi wa kwanza huru nchini Somalia kwa miaka 42 tangu Mohamed Siad Barre kuchukua mamlaka mwaka 1969.
Rais Mohamud,mwmenye msimamo wa kadri, aliapishwa mara moja baada ya kutangazwa kuwa alimshinda bwa Ahmed kwa wingi wa kura. Wabunge wapya wa Somalia ndio waliopiga kura.
"Naahidi kuwa Somalia inachukua nafasi yake katika jamii ya kimataifa kuanzia leo na kwa kufanikisha hilo,lazima tuhakikishe tunapiga hatua mbele.'' alisema rais mpya katika hotuba yake ya ushindi.
Waziri mkuu wa Uingereza pamoja na balozi wa umoja wa mataifa kuhusu Somalia, Augustin Mahiga wameonya kuwa bado jukumu kubwa linasalia kuhusu Somalia.
Kulikuwa na wagombea 22 kwenye uchaguzi huo, akiwemo Rais anayeondoka Shariff Sheikh Ahmed na waziri mkuu Abdiweli Mohamed Ali.
Hassan Sheikh Mohamud alishinda kufuatia duru ya tatu ya upigaji kura, ambapo alikuwa anachuana na Rais anayeondoka Shariff Sheikh Ahmed.
Katika raundi ya kwanza Sheikh Ahmed alikuwa amepata ushindi mwembamba wa kura 64 dhidi ya 60 alizopata Sheikh Mohamud.
Kwa jumla wabunge 271 walipiga kura.
Katika duru ya mwisho wabunge wengi waliowaunga mkono wagombea waliochujwa walimuunga mkono Sheikh Mohamud , akapata kura 190 dhidi ya 70 alizopata Rais anayeondoka.
Hii ni mara ya kwanza kwa uchaguzi wa Rais kufanyika katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu, tangu kuondolewa kwa serikali ya kijeshi mwaka 1991.

No comments:

Post a Comment