Friday, December 14, 2012

Ya Ray C na Kikwete Yameleta Mambo

 
Soma Hapa...ASSALAM aleykum mheshimiwa. Pamoja na majukumu mengi yanayokukabili, nimeona ni nafasi yangu nzuri kuwasiliana nawe na ninajua utaisoma barua hii kwa sababu kadhaa ambazo nitazieleza hapa chini.

Dhumuni la barua hii ni kukueleza kuhusiana na mwanadada Rehema Chalamila ‘Ray C’, hakika umeonyesha unajali na umeonyesha wewe ni rais wa watu. Angekuwa m

wingine angeamua kunyamaza na mwanadada huyo angepotea, hakuna ambaye angejali.

Lakini najua leo, wapo watakaokulaumu na kutaka kulalama kwamba mbona wengine haujawasaidia? Wala usijali kwa kuwa hauwezi kuwafurahisha watu wote, ingawa mimi nataka kutumia nafasi hii kukukumbusha angalau kidogo.

Nakukumbusha mheshimiwa kwamba, umeyasahau magazeti pendwa, hasa yanayochapishwa na Kampuni ya Global Publishers Ltd, ambayo ndiyo yalifanya kazi kubwa ya kumfikisha Ray C mikononi mwako hadi ukagundua ukubwa wa tatizo lake.

Lakini hata wakati wa utoaji shukurani, nilifikiri Ray C na mama yake wangeweza kuyashukuru magazeti pendwa ya Global Publishers ambayo ndiyo yalikuwa ya kwanza kuanika matatizo hayo makubwa ya Ray C hadi wewe ukachukua hatua.

Wakati unachukua hatua, nilifurahi sana. Unajua nini kilinifurahisha mheshimiwa? Baada ya kugundua nawe ni msomaji wa magazeti pendwa ya Global Publishers. Wapo wanaoyadharau, sasa kama hadi wewe unasoma, huyo mwenye jeuri ya dharau ni nani? Hapo nakupa tano.

Sitaki kulazimisha magazeti pendwa yapewe tuzo, ila nakumbusha tu ili kuonyesha kazi ya Watanzania halisi kama hawa waliomo Global Publishers inathaminiwa. Maana nakumbuka mara baada ya stori na picha za kwanza za Ray C akiwa amelala kwenye bajaji, wapo watangazaji wa redio ya Clouds walishambulia magazeti ya Global, eti yametumwa.

Ajabu nao leo kila siku wanazungumzia hali ya Ray C! Nahisi baada ya mwanadada huyo kufika kwako, watakuwa hawana la kusema na kama ni aibu wanayo na wameihifadhi, wanaitumia taratibu kwa faida zao. Walikuwa wanajua matatizo yake, wakaona kuyaficha ndiyo kitu kizuri, walikubali afe. Magazeti pendwa yakakataa na kumfikisha mikononi mwako.

Wapo watu wa Clouds walielewa hilo lakini hata niliposikia wanazungumza na kupongeza, pia walitaja magazeti bila ya kusema ni ya Global Publishers ambayo ni maarufu kama udaku.

Mheshimiwa, picha za Ray C akiwa teja kamili kwenye bajaji, sisi vijana huku mtaani tunaita kubembea, hakika zilikuwa zinatia huzuni sana. Naamini ndiyo maana zilikugusa, ila nikuambie mchezo ulikuwa mgumu hadi kuzipata na ilikuwa kazi ya zaidi ya miezi kadhaa hadi kumvizia akiwa vile.

Ndiyo maana wengine wakashindwa kwa kuwa taarifa zao ni za kwenye vikaratasi maarufu kama ‘press realize’, au mkiwaalika kwenye ‘press conference’ ambako mara nyingi wanatoka na ‘lead story’ halafu wanapewa sifa za kuwa ‘serious’.

Mnaowaamini wako ‘siriaz’ hawafanyi kazi ya habari za uchunguzi, lakini kuna taarifa nyingi zinaanzia Global Publishers na baada ya hapo mnaowaona wako makini wanazidakia lakini nao kwa ujanja hawataki kuipongeza au hata kuitaja GPL.

Wasaidizi wako nao kama umewaita waandishi, hata siku moja hawataki kuwaalika waandishi au wahariri kutoka GPL, lakini nashangaa ilikuwaje safari hii hadi ‘newspaper’ likapenya na kukufikia halafu ukamuona Ray C alivyokuwa akiteketea.

Silazimishi mualiko, sina haja ya kusisitiza kuhusiana na tuzo kwa kuwa niliamua kujitoa baada ya kugundua hadi wale wanaozitoa wanaangalia waandishi kutoka serikalini, redio na magazeti ya chama au yale yanayoitwa yako ‘siriaz’ kwa habari za press conference!

Hapa tuna Championi, hili unalolisoma sasa. ‘Linakimbiza’ (kwa kuwa ni mwanampira wa kikapu najua unaelewa neno hili) vibaya, yapo yanayojiita magazeti kongwe, yamepotezwa kabisa na inafikia tunauza hadi magazeti mara tatu yao, lakini wanajaribu kutufunika kwa kisingizio cha ‘siriaz’.

Nimefanya kazi Habari Corporation (Dimba-halafu nikawa mmoja wa waanzilishi wa Bingwa), nikahamia Mwananchi (nilikuwa Mwanaspoti), acha mheshimiwa, kule nilikimbiza vibaya, wasomaji ni mashahidi wangu.

Ila hakuna sehemu niliyofanya kazi na watu wanaojituma, wabunifu na wenye uwezo kama hapa Championi, ndiyo maana unaona habari kama za Ray C zinatokea hapa nilipo.

Najua siku moja tutakutana (Mungu akipenda), sina haja ya kumueleza kitu Ridhwani ambaye nakutana naye mara kibao, pia ni mshikaji wangu, ila nikikuona nitakuhadithia zaidi ili ujue Global Publishers wanayolazimika kuibeza ni zaidi ya unavyoifahamu na imefanya mengi makubwa. Hilo la Ray C ni asilimia moja tu.

Natamani kuendelea kuandika, lakini najua una majukumu mengi kwa kuwa Tanzania ni kubwa. Acha nikupe nafasi, ila nakukumbusha mheshimiwa na najua utakubaliana nami kwamba kazi ya Global Publishers ingekuwa inafanywa na kampuni ya Wazungu kutoka Ulaya au Wakenya, basi Watanzania wenzangu wangesifia na kujikomba kweli.
Tukionana, tutachambua zaidi.
Heshima na salamu,

Source: GPL

No comments:

Post a Comment