Mh.Mbowe katika harakati. |
Katika barua hiyo ya Septemba 10, mwaka huu, iliyoandikwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, pamoja na hatua nyingine CHADEMA imetaka Rais Kikwete achukue hatua ya kuwafukuza kazi baadhi ya viongozi.
Wanaotakiwa kufukuzwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, IGP Said Mwema, Kamishna wa Operesheni wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja, RPC wa Mkoa wa Morogoro, Faustine Shigolile na RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda, kwa kutowajibika kufuatia mauaji yaliyotokea katika mikoa ya Morogoro na Iringa.
Aidha, CHADEMA kimetaka Rais Kikwete aunde tume ya kijaji/kimahakama ya uchunguzi wa vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa yaliyohusisha chama hicho.
Vifo hivi ni vile vilivyotokea Arusha Januari 5, mwaka jana, Igunga Novemba mwaka huo huo, Arumeru Mashariki Aprili mwaka huu, Iramba Julai 14, Morogoro Agosti 27 na Iringa Septemba 2, mwaka huu.
Kwamba wakati wakisubiri hatua za rais pamoja na majibu ya barua hiyo, wanawaagiza viongozi na wanachama wake kutokutoa ushirikiano kwa kamati iliyoundwa na Waziri Nchimbi na timu zilizoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza mauaji yaliyofanywa na askari katika mikoa ya Iringa na Morogoro.
Katika barua hiyo, Mbowe aliongeza kuwa hivi karibuni mkoani Iringa wakati wa kufungua matawi ya chama chake kwenye Kata ya Nyololo, polisi walimlipua kwa bomu mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi.
Alisema kuwa pamoja na polisi kuhusika na mauaji hayo, bado Waziri Nchimbi, IGP Mwema, Kamanda Chagonja, makamanda Shigolile na Kamuhanda hawakuchukua hatua yoyote ya kuwajibika kwa kuhusika moja kwa moja na matukio haya au kiutendaji katika jeshi hilo kwa ujumla.
“Ili kupata ukweli wa sababu za vifo hivyo, mauaji yote haya hayajafanyiwa uchunguzi wowote wa kimahakama/kijaji kwa mujibu wa sheria za nchi yetu kinyume na ahadi ya waziri mkuu bungeni wakati akihitimisha hoja yake katika Bunge la Bajeti la mwaka 2011/2012. Hakuna uchunguzi wa kifo ‘inquest’ uliofanyika na hakuna Mahakama ya Korona ‘Coroner’s Court’ iliyoanzishwa ili kuchunguza vifo hivi,” alisema Mbowe.
Kwamba Kamati Kuu ya CHADEMA katika kikao maalumu hivi karibuni, mojawapo ya mambo yaliyoazimiwa ni kumwandikia barua rais kwa lengo la kumtaka achukue hatua za utekelezaji kwa mujibu wa mamlaka yake na kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Iwapo serikali haitazingatia, CHADEMA kitawaongoza wananchi kwa njia za kidemokrasia, ikiwemo maandamano ya amani kushinikiza hatua za haraka kuchukuliwa kwa masilahi ya taifa,” alisema Mbowe.
Aliongeza kuwa katika majadiliano ya kina kabla ya kufikia maazimio na maamuzi hayo, kamati kuu ilizingatia kuwa hali ya siasa nchini ni tete, serikali inayoongozwa na CCM imeshindwa kusimamia vizuri rasilimali za nchi ikiwamo kudhibiti mfumuko na ongezeko la bei, hivyo kuchangia ugumu wa maisha kwa wananchi na migogoro ya kijamii na ufisadi nchini.
No comments:
Post a Comment