Tuesday, September 18, 2012

Mnyika amvaa Waziri Tibaijuka,anahisi kuna Ufisadi unanukia

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (CHADEMA), amemtaka Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kuueleza umma kuwa mwendelezaji mwenza aliyepatikana kwa ajili ya mji wa kisasa wa Luguruni anatoka kampuni gani.
Mbali na kueleza jina la kampuni hiyo, Mnyika pia amemtaka waziri huyo kueleza kazi hiyo itaanza lini na nafasi ya serikali na wananchi ni ipi katika mradi huo na kisha aweke hadharani mkataba ulioingiwa baina ya mwendelezaji mwenza huyo kutoka sekta binafsi na serikali, ili wananchi watambue mipaka yao.
Mnyika alitoa kauli hiyo juzi katika eneo la Kibamba mji mpya alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara, baada ya kufanya kazi ya kichama ya kufungua matawi saba ya CHADEMA katika kata ya Kwembe.
Alisema serikali ilichagua eneo la Luguruni kuwa moja ya sehemu zitakazojengwa miji ya kisasa kwa lengo la kupunguza msongamano mjini na ikaingia gharama za kupima viwanja kulipa fidia kwa wananchi wa maeneo hayo na kueleza kuwa kitendo cha kuacha kuwa pori ni kuhatarisha usalama wa wananchi wa maeneo hayo.
“Mwaka huu serikali iliahidi bungeni juu ya kupatikana mwendelezaji mwenza sasa watufahamishe basi ni nani kwa kuwa leo wananchi wanalalamikia eneo hili kuwa sehemu ya maangamizi yao, wanakabwa wanaibiwa na hata kubakwa kama walivyosema lakini pia kuendelea kuacha eneo hili kuwa pori ni kuwaruhusu watu wavamie kisha serikali iingie gharama nyingine ya kuwaondoa,” alisema Mnyika.

No comments:

Post a Comment