MTU mmoja anayeshukiwa kuwa ndiye aliyehusika kumpiga risasi na kumuua
aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow (53),
amekamatwa na polisi mkoani Mwanza.Kamanda Barlow aliuawa kwa kupigwa
risasi shingoni usiku wa manane wakati akimsindikiza mwanamke mmoja
baada ya kuhudhuria kikao cha harusi ya ndugu yake.
Mtuhumiwa huyo
anaaminika kuwa ndiye aliyehusika na kumpiga risasi, na inadaiwa kuwa
ana rekodi ya kuhusika na matukio mbalimbali ya uhalifu.
Ilielezwa kuwa mtuhumiwa huyo kabla ya kuhusika na mauaji hayo, alitoka jela miezi minne iliyopita.
Habari
za uhakika kutoka ndani ya jeshi hilo pamoja na timu ya makachero
wanaohusika na uchunguzi wa mauaji hayo chini ya Mkurugenzi wa Upelelezi
wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, zimeeleza kwamba, kukamatwa
kwa mtuhumiwa huyo kumetegua kitendawili cha chanzo cha mauaji hayo na
kubainisha kuwa hayahusiani na mapenzi.
“Jana (juzi) ilikuwa ni siku
muhimu kwa Jeshi la Polisi, mtu muhimu sana katika sakata la mauaji
hayo alikamatwa, huyu kwa mujibu wa rekodi zetu anaonekana kuhusika na
matukio kadhaa ya ujambazi na kabla ya ya mauaji ya kamanda wetu alikuwa
jela,” kilieleza chanzo chetu.
Kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo, kunafanya waliokamatwa hadi sasa kufikia sita akiwamo Mwalimu Dorothy Moses.
Imeelezwa
kwamba kupatikana kwa mtuhumiwa huyo, maelezo ya awali ambayo
yalitolewa na Mwalimu Dorothy Moses pia yamebadilika kutokana na
kuonekana ni mmoja wa watu wa karibu na mtuhumiwa huyo na kwamba zipo
dalili za kuhusika katika njama hizo za mauaji.
Kaimu Kamanda wa
Polisi mkoani Mwanza, Lili Matola alikiri kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo,
lakini hakutaka kuingia ndani kwa madai ya kwamba hiyo ilikuwa ni kazi
ya DCI Manumba anayehusika na upelelezi huo.
“Naomba muwe na subira,
mambo ni mazuri, kwani hatua za upelelezi wa mauaji ya Kamanda Barlow
umefikia hatua nzuri, hayo mnayosema baadhi ni sahihi, lakini mengine
nami nayasikia, ila tu la muhimu tuvute subira kwani ukweli wote
utatangazwa,”alieleza.
Kutokana na uchunguzi huo kuingia katika
hatua muhimu, ilielezwa kwamba DCI Manumba aliwasiliana na Mkuu wa Jeshi
la Polisi nchini, (IGP) Said Mwema ambaye aliwasili jana jijini Mwanza.
Baadaye
Mwema aliiwasilisha ripoti ya kukamatwa kwa mtuhumiwa katika kikao cha
Kamati ya Ulinzi na Usalama cha Mkoa wa Mwanza chini ya Mkuu wa Mkoa
Mhandisi Evarist Ndikilo.
chanzo -mwananchi
No comments:
Post a Comment