NIMESHINDWA kuamini kama habari zilizovuma kwenye vyombo vya habari
jana zikimkariri Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, akilalamikia
mambo kadhaa ndani ya chama chake kama zimetoka kinywani mwake.
Na labda nichukue fursa hii kuwatahadharisha tena wanasiasa wa ndani
ya CCM na watendaji wa serikali yake, wanaofanya kazi karibu sana na
rais huyu. Wengi wamejikuta majeruhi wa siasa zake kwa kuwa anachokisema
mdomoni sicho kilichoko moyoni.
Samwel John Sitta atakuwa shahidi wangu wa kwanza maana nilitumia
makala nzima kumwonya na kumtahadharisha juu ya kitendo cha JK kwenda
mpaka Urambo kuzindua ofisi ya mbunge wa Urambo na kumwaminisha kwamba
yuko pamoja naye katika harakati zake za kugombea tena ubunge na
hatimaye uspika.
Nilimwambia kwamba asiyumbe akaacha kusimamia utekelezaji wa serikali
kwa maazimio ya Bunge kuhusu kashfa ya Richmond. Alinisikia, lakini
hakunielewa, muulize alivyokujakulia baadaye akidai eti sifa zote za
kuwa spika alikuwa nazo isipokuwa moja tu: “awe ni mwanamke.”
Na hii moja haijatamkwa kwenye katiba wala kwenye sheria yoyote ya
nchi wala kwenye kanuni za Bunge, wala kwenye kanuni zozote, bali
maazimio ya kikao kilichoongozwa na JK, na pengine maazimio yake kupitia
kwenye kikao.
Jana kaibuka na kali zaidi. Gazeti dada la hili, jana lilisema:
Makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yanaonekana kumwelemea
Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete, na sasa ameamua kutumia
mkutano mkuu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (UWT), kukemea vitendo vya
kudhalilishana na makundi wakati na baada ya uchaguzi.
Rais Kikwete pia alionya juu ya vitendo vya rushwa vinavyozidi
kushamiri ndani ya chama hicho akisema kuwa visipochukuliwa hatua
mapema, kuna hatari ya kukifikisha chama katika hatua mbaya.
Gazeti lilisema akifunga mkutano huo wa nane wa uchaguzi UWT, Rais
aliwataka kufanya jitihada za kupunguza mgawanyiko uliotokea baada ya
uchaguzi wao uliomalizika hivi karibuni.
Alisema imekuwa ni hulka sasa hasa baada ya kumalizika uchaguzi kwa
wanachama kuendeleza na kuwekeana uhasama kama uliokuwepo wakati wa
kampeni.
“Itakuwa ni aibu sana na ajabu, pia utakuwa hujatenda haki kwa
kumbagua ambaye hakukuchagua; natolea mfano kwangu katika uchaguzi
uliopita, Prof. Mark Mwandosya hakushinda, lakini kwenye serikali yangu
nilimuweka licha ya kuwa nilifanyiwa mambo ya ajabu sana ambayo ni
vigumu kuyavumilia, lakini kwa mwanasiasa, lazima uwe mkomavu.
“Kweli tusipokemea vitendo hivi na kuviacha vikiendelea, tutakipeleka
chama mahali pabaya, ninasikitika sana kusikia hata wanawake sasa
wanajihusisha na utoaji rushwa ili kununua nafasi za uongozi kitu
ambacho ni hatari sana,” alisema Kikwete.
Alifafanua kuwa chama kinakoelekea si kuzuri ni lazima zifanyike jitihada za mabadiliko.
Mahali kwingine nimesema kwamba hakuna rais aliyepata bahati ya
uongozi wa taifa hili wakati wa vyombo vingi vya habari, kama Kikwete.
Ni kweli kwamba uhuru kamili wa vyombo hivi vya habari bado ni ndoto,
lakini umeongezeka kwa nguvu kutokana na kuongezeka kwa vyombo vyenyewe.
Ni kwa sababu hiyo vimejitokeza vyombo kadhaa kama gazeti hili ambavyo
vinaiweka nchi mbele daima na kusimamia ukweli na hivyo kuweza kusema
ukweli bila kuogopa.
Kikwete ni rais ambaye amevunja rekodi ya kuelezwa ukweli, kuaswa,
kukosolewa, kupewa maoni, kukanywa na hata kuelekezwa mambo mengi katika
utawala wake kiasi kwamba angesoma na kufuata hata nusu tu ya yale
anayoandikiwa kwenye vyombo vya habari, angekuwa rais bora kuliko wote
ikizingatiwa nguvu kubwa ya sapoti ya Watanzania iliyomwingiza
madarakani kwa mara ya kwanza kwa asilimia 80.2.
Katika utawala wake, hakuna kitu kimepigiwa kelele na JK kushauriwa
mara nyingi kama suala la mtandao uliomwingiza madarakani. Katika marais
wote wanne walioongoza taifa hili, hakuna rais aliwahi kuutafuta urais
kwa udi na uvumba kama Rais Kikwete. Mwalimu Nyerere alipambana kutafuta
uhuru na uhuru ulipopatikana akajikuta anachaguliwa yeye kuwa Waziri
Mkuu. Baadaye baada ya nchi kuwa jamhuri kamili pia wenzake walimwona
wakamwambia unafaa kuwa rais wetu.
Alipong’atuka Mwalimu na zamu ikawa ni ya Zanzibar, wazee wa Zanzibar
walimpendekeza Ally Hassan Mwinyi na akapigiwa kura kuwa rais wa
Jamhuri. Baada yake hakuna aliyetegemea kwamba Benjamin Mkapa angekuwa
rais. Watani wake walipenda sana kumtania kwamba Kenneth Mkapa, mchezaji
beki namba tatu wa timu ya Yanga wakati huo alikuwa ni maarufu kuliko
Benjamin Mkapa. Lakini wenzake walimwona ikiwa ni pamoja na Mwalimu.
Wakamshawishi kuchukua fomu, wakampigia debe na hatimaye akawa rais
wetu baada ya kumshinda Kikwete ambaye aliingia kwenye kinyang’anyiro si
kwa kuombwa na watu, bali kwa kuutamani yeye urais akakaa chumbani yeye
na mwenzake Lowassa na wakakubaliana kwamba wachukue fomu halafu
atakayekuwa rais amteue mwenzake kuwa waziri mkuu.
Baada ya kushindwa na Mkapa, ndipo alipofanya kitu cha ajabu ambacho
hakikuwahi kufanyika hapa nchini na sasa nashangazwa na pale anapojidai
anasikitishwa nacho. Wakati Mkapa akihangaika huku na kule kujenga
uchumi wa nchi kwa miaka kumi ya uongozi wake, Kikwete alikuwa busy
kuunda kundi la mtandao ambalo naamini kabisa lilifikia mahali pa
kumtengenezea umaarufu ambao hata hakuwa nao ili tu aje kushinda urais
2005.
Ninaamini ndani ya dhamiri yangu kwamba kundi la mtandao lilitumia
kila aina ya njia, halali na haramu, katika kufanikisha mpango wake wa
kumwingiza Kikwete Ikulu. Moja ya njia ni kugawa wanachama na viongozi
wa chama chake katika makundi kama alivyosema kwamba kundi la Mwandosya
lilipambana naye. Ya pili ilikuwa ni kutumia rushwa kama ambavyo
ameshindwa kukanusha habari za viongozi wa vyama vya upinzani kwamba
pesa za EPA zilizoporwa Benki Kuu zilitumika kumwingiza madarakani.
Mkakati mwingine haramu ulikuwa ni kutumia vyombo vya habari kuandika
habari za hovyo juu ya wagombea wenzake, hata kama hazina ukweli kama
ambavyo waziri mkuu wa wakati huo, Sumaye, alipofikia mahali akasema
“mtu anayetumia kalamu kuwadhibiti wapinzani wake, akishachukua madaraka
atatumia risasi kuwadhibiti.”
Hayo ni ya kabla ya kampeni na uchaguzi. Baada ya uchaguzi mtandao
uliendelea na kazi yake. Baada tu ya uchaguzi wa 2010 na Samwel Sitta
kupigwa dafrau uspika kitendo kilichomfanya kuanza kuwalalamikia wenzake
kwamba ni mafisadi ndo wamemwangusha, gazeti moja linalomilikiwa na
kada maarufu wa CCM, lilidiriki kutamka kwamba ugomvi wa Sitta na
anaowaita mafisadi unatokana na kunyimwa uwaziri mkuu mwaka 2005.
Kwa hiyo baada ya uchaguzi 2005 mtandao ulifanya kazi nyingine haramu
ya kugawa vyeo kwa walioshiriki tendo haramu la kumwingiza Kikwete
madarakani kwa nguvu. Na hapo hapo wakiwabadilishia wengine vyeo
walivyoahidiwa huku wakiwanyima wengine vyeo walivyoahidiwa.
Kitu hicho kilisababisha mgawanyiko na chuki miongoni mwao na mtandao
kuvunjika na kuundwa mitandao mingine kadhaa kuelekea 2015. Ni hiyo
ambayo sasa inakiumiza sana chama chake. Lakini si hivyo tu, wana CCM
walianza kujifunza kwamba kumbe ukitaka kupata uongozi unaoutamani, unda
mtandao.
Tafuta fedha nyingi, honga watu: wanachama, viongozi, wanahabari na
hatimaye wananchi. Utapata kura za asilimia 80 na kuendelea. Kama huna
pesa usijali. Ili mradi una nafasi ama mzazi wako ama ndugu yako ana
nafasi ya kushika mali ya umma, pora hiyo mali ya umma maana haina
mwenyewe uitumie kujiwekea mazingira mazuri mbele ya safari.
Inashangaza leo Kikwete anazungumza akijidai anazungumza kwa uchungu
sana. Waandishi na wachambuzi mbalimbali tulimwambia. Tulimweleza kwamba
alichoanzisha ni sawa na ‘kula nyama ya mtu’. Si yeye wala wenzake
ndani ya chama watakaoacha. Wote wataendelea na dhambi hiyo na chama
kitakufa kikiwa kimeshaidhoofisha sana nchi!
Si siri hata CHADEMA wakiingia madarakani 2015 watahitaji kufanya kazi
ya ziada kuirudisha nchi kwanza kwenye pointi sifuri ya maendeleo maana
kwa sasa iko hasi kabisa kutokana na matendo haya ya akina Kikwete.
Tulimwambia avunje kundi lake na kila aliyekuwa ndani ya kundi ambaye
badala ya kufanya siasa za kistaarabu za kujenga hoja alijiingiza katika
rushwa na matumizi mabaya ya vyombo vya habari na kibaya zaidi kupora
mali ya umma, apelekwe mahakamani.
Kwa kuwa alijua akiwapeleka mahakamani waliopora pesa za EPA watamtaja na yeye, akaamua kuweka pamba masikioni.
Ndiyo maana nilifikia mahali nikakubali kwamba Kikwete ni Chaguo la
Mungu. Katumwa na Mungu kuiua CCM kwa maslahi ya taifa. Rais wangu na
mwenyekiti wa chama kikongwe, usilie. Kuutoa mwiba kwenye mwili lazima
kulete maumivu makali. Vumilia! CCM inajimaliza mbele ya Watanzania.
Itatolewa kwenye uongozi kama mwiba utolewavyo mwilini. Subiri
ikishapigwa chini, ustaafu na kuwaachia akina Nape kama wanaweza
waijenge upya itarudi madarakani kama wananchi wataona kweli
imebadilika. Maneno ya “chama kitafika pabaya” ni ya kuwapaka wanachama
mafuta kwa mgongo wa chupa. Waeleze wazi tu kwamba chama kimeshafika
pabaya na kiukweli 2015 kinang’oka madarakani. Kwa kuwaeleza ukweli,
watajiandaa
kalamu ya mwigamba-Tanzania daima
No comments:
Post a Comment