Monday, October 8, 2012

Je ni kweli Dk.Ulimboka Hajafungwa mdomo?

MWENYEKITI wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, Dk. Stephen Ulimboka, amejitokeza na kuzungumzia mustakabali wake huku akisisitiza kuwa kamwe hajafungwa mdomo bali anajipanga kuanika ukweli wa kile kilichomsibu.
Dk. Ulimboka ambaye alitekwa, kuteswa, kuumizwa vibaya na kisha kutelekezwa katika msitu wa Mabwepande nje kidogo ya jiji la Dar es Salaamu usiku wa kuamkia Juni 27 mwaka huu, amekuwa kimya baada ya kurejea nchini akitokea Afrika Kusini alikokwenda kwa matibabu zaidi.
Tangu kurejea nchini mapema Agosti, Dk. Ulimboka amekuwa mafichoni kutokana na kile kilichoelezwa ni kutotaka wabaya wake wajue alipo ili wasijewakamdhuru na kupoteza ushahidi hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa akiwataja hadharani baadhi ya maofisa wa Usalama wa Taifa akidai walishiriki kumteka.
Hata hivyo, ukimya wake umeibua mjadala kiasi cha watu wengine kuanza kudhani kuwa amenyamazishwa asisema chochote juu ya tukio hilo ambalo limelighubika taifa kutokana na mkanganyiko uliyopo.
Akizungumza na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam jana baada ya ukimya huo, Dk. Ulimboka alisema kamwe hawezi kuzibwa mdomo kama ambavyo taarifa za uvumi zilivyozagaa.
Alisema kuwa muda ukifika atazungumzia masuala yote yanayohusiana na kutekwa kwake na hatua gani zitakazofuata.
“Siwezi kuzibwa mdomo na yeyote, hata walionichagua kuwa mwenyekiti wao, wanafahamu hivyo, suala ni wakati tu, utakapofika hasa baada ya kukamilisha masuala ya kisheria, nitazungumza hivi karibuni ili kuondoa hofu hiyo,” alisema.
Dk. Ulimboka pia amewataka wanataaluma wenzake kutulia hasa kwa wakati huu ambao bado ameweka kipaumbele katika tiba yake ambayo ameielezea kuendelea kuimarika na kwamba madai yao bado ni ya msingi na kamwe hayawezi kuishia hapo yaliposimamia.
Kutekwa na kuteswa kwa Dk. Ulimboka kulitokea katikati ya mgogoro wa madaktari na serikali ambao uliibua mgomo uliotikisa nchini, jambo ambalo lilisababisha serikali kuwa lawamani ikihusishwa na tukio hilo licha ya viongozi wake kukanusha.
Baada ya kulazwa kwa muda katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk. Ulimboka alipelekwa nchini Afrika Kusini Juni 30 kwa matibabu zaidi alikolazwa kwa takriban mwezi mmoja na siku kadhaa kisha kurejea akiwa na afya njema na kupokelewa kwa kishindo huku akiahidi kuzungumzia mustakabali mzima wa tukio hilo.
Lakini baada ya hapo, Dk. Ulimboka amekuwa kimya jambo ambalo limezua minong’ono mingi katika jamii kiasi cha wengine kudai kuwa ‘amefumbwa mdomo’ na kuwasaliti madaktari wenzake.

No comments:

Post a Comment