HOTUBA ya Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) akisifu utendaji
kazi wa Rais Jakaya Kikwete na kwamba wananchi wa Rombo wana imani naye
kubwa jana ilimkuna Rais Kikwete.
Katika hotuba yake katika sherehe
za uzinduzi wa Barabara ya Mkuu-Tarakea, Selasini alisema wapo wanasiasa
ambao hakuwataja wenye desturi ya kupanda kwenye migongo ya mafanikio
ya wenzao.
Alisema kama angekuwa na uwezo angeipa barabara hiyo jina
la “barabara ya JK” kwa sababu ndiye aliyetoa fedha za ujenzi wa
barabara hiyo na kuhakikisha ndoto ya wananchi wa Rombo inatimia.
“Nina
kila sababu ya kukushukuru na kukupongeza kwa sababu wapo wanasiasa
wamekuwa na desturi ya kupanda kwenye migongo ya wengine wamekuwa
wakisema wamejenga hii barabara”alisema.
Alisema barabara hiyo
imekuwa katika makabrasha tangu enzi za ukoloni. lakini ni Rais Kikwete
ambaye ametimiza ndoto ya Warombo ya kuungana tena na wenzao kwa
shughuli za kibiashara.
Selasini alisema Wananchi wa Rombo
walikuwa kama wametengwa na wananzi wenzao wa wilaya nyingine kwa vile
walikuwa wakitumia siku zaidi ya saba kutoka Tarakea hadi Moshi mjini.
Mbunge
huyo alimuomba Rais Kikwete asaidie kujenga malambo mawili kwa ajili ya
kilimo cha umwagiliaji na pia kikosi cha kudhibiti tembo kutoka Kenya
kipatiwe gari la doria.
Alisema Rais Kikwete ndiye aliyetoa ahadi ya
kuijenga barabara hiyo ambayo huko nyuma iliwahi kutolewa ahadi nyingi
za kujengwa lakini hazikuweza kutekelezwa hadi Rais Kikwete alipoivalia
njuga.
Kwa mujibu wa Selasini,wananchi wake wana imani kubwa na
utendaji wa Rais Kikwete katika kipindi cha miaka mitatu iliyobaki na
akasema kwa ujenzi wa barabara hiyo kamwe hawatamsahau maishani.
Katika
hotuba yake, Rais Kikwete alisema Selasini ni mfano mwema wa siasa na
akasema anaposemea mahitaji ya Wananchi wa Rombo anaiambia Serikali na
kuahidi kutekeleza ombi lake la malambo.
“Nakushukuru kwa maneno yako
mazuri wewe ni mfano mwema wa siasa za vyama vingi, hakuna neno zuri
bali kuna wanaotawala na wako wanaopika utawala”,alisema Rais Kikwete
bila kufafanua.
Alisema haitakuwa na maana kwamba kila kizuri
kinachofanywa na Serikali basi viongozi wa upinzani wakibeze akisema
angeshangaa kama wapinzani watakataa hajajenga barabara hiyo
Rais
Kikwete alisema kuzinduliwa kwa barabara hiyo iliyojengwa kwa usimamizi
wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kutafungua fursa za kiuchumi
kwa wananchi wa Rombo na nchi jirani.
No comments:
Post a Comment