MADIWANI wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
katika Manispaa ya Moshi, Kilimanjaro juzi walitwangana makonde huku
kiini kikitajwa kuwa ni gari la Mstahiki Meya.
Tukio hilo
linadaiwa kutokea juzi katika moja ya kumbi za mikutano ndani ya
Halmashauri ya Manispaa ya Moshi wakati madiwani hao wakiwa katika kikao
cha ndani cha maandalizi ya mkutano wa baraza la madiwani.
Hata hivyo, licha ya taarifa za tukio hilo kuzagaa haraka, wahusika wameifanya siri ili kulinda heshima ya chama hicho.
Inadaiwa
kuwa kisa cha kupigana ni ubishi juu ya nani anastahili kupanda gari
hilo la Meya na baada ya kurushiana maneno, madiwani hao walivaana na
kuanza kupigana kabla ya kuamuliwa na wenzao.
Habari zinadai kuwa
madiwani watatu wamekuwa wakilitumia gari la Meya kila wanapolihitaji
bila kikwazo jambo ambalo limekuwa likiwakera baadhi yao.
Mwenyekiti
wa Madiwani wa CCM katika Baraza hilo, Michael Mwita amekiri kuarifiwa
juu ya tukio hilo lakini hakulishuhudia akisema alikuwa katika ukumbi
mwingine.
Meya wa Manispaa ya Moshi, Jaffar Michael hakupatikana
kuzungumzia tukio hilo kwani tangu juzi, simu yake imekuwa ikiita bila
kupokewa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Bernadette Kinabo alisema amesikia kutokea kwa tukio hilo.
Alisema
tukio hilo limemsikitisha na kuwataka madiwani kuhimili jambo hata kama
ni kutukanwa... “Nimearifiwa juu ya jambo hilo japo si kwa undani sana.
Ila kwa kweli madiwani wanapaswa kujiheshimu ili na wengine wajifunze
kutoka kwao. Haipendezi madiwani kutumia lugha ya kuudhi zaidi yao na
anayetolewa lugha hiyo naye lazima azuie jazba.”
Mwenyekiti Chadema achomwa mkuki
Mwenyekiti wa Chadema, Tawi la Mwawaza, Shinyanga, Bundala Katunge amechomwa mkuki baada ya kuvamiwa na
kushambuliwa na kundi la watu zaidi ya 30.
Tukio hilo lilitokea juzi katika Kijiji cha Mwawaza saa tano usiku akiwa amelala nyumbani kwake.
Mashuhuda
wa tukio hilo walidai kuwa Katunge alijeruhiwa baada ya kutoka nje ya
nyumba yake mara baada ya kusikia bendera ya Chadema ikishushwa kwenye
mlingoti.
Ilidaiwa kuwa alijaribu kuwazuia lakini walimzidi nguvu
na kuanza kumshambulia. Aliwaponyoka na kuanza kukimbia ndipo mmojawao
alipomrushia mkuki na kumchoma sehemu za mbavu upande wa kushoto. Baada
ya tukio hilo kundi hilo lilitoweka.
Katibu wa Chadema Wilaya ya
Shinyanga, Nyangaki Shilungushela alisema Katunge alikimbilia kwa
majirani ambao walimpeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga ambako
alifanyiwa upasuaji na kulazwa akisema hali yake ni mbaya.
Mganga
Mfawidhi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Frederick Mlekwa alikiri kuwapo kwa
mgonjwa huyo na kusema anaendelea kupatiwa matibabu.
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema hana taarifa ya tukio hilo.
Hata
hivyo, wananchi wa eneo hilo walisema jana kwamba tangu tukio hilo
lilipotokea, hawajaona polisi aliyefuatilia licha ya kutoa taarifa na
kupewa fomu namba tatu iliyowezesha matibabu ya kiongozi huyo wa
Chadema.
“Tunashangaa ni kwa nini polisi hawajatoa ushirikiano na
huku taarifa wameshazipata,” alisema mmoja wa wakazi wa kijiji hicho
ambaye hakutaka jina lake litajwe.
CHANZO GAZETI LA MWANANCHI
No comments:
Post a Comment