POLISI nchini wamepanga kusambaratisha mtandao unaodhamini na kuchapisha
vipeperushi vinavyohamasisha kufanyika kwa maandamano, kutaka kutolewa
kwa Katibu wa Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda na wenzake.
Hatua
hiyo imekuja baada ya waumini hao kupanga kufanya maandamano Novemba
Mosi, ambayo yatahamasisha mahakama hiyo kutoa dhamana kwa kiongozi wa
taasisi hiyo na wenzake.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Suleiman
Kova alisema wataanza kufanya msako wa wote wanaohamasisha,
wanaochapisha na wanaotoa vipeperushi ili kuwakamata.
“Tunafuatilia wadhamini na wachapishaji wa vipeperushi kwani ni chanzo cha uchochezi na upotevu wa amani nchini,” alisema Kova.
Kova
alisema maandamano hayo ambayo yamepangwa na waumini hao yanatishia
amani , wananchi watashindwa kwenda kazini na kurudisha nyuma maendeleo
ya nchi.
“Hatuna mazungumzo tena kwa suala lolote litakalotishia
uvunjifu wa amani hasa kwa yeyote atakayefanya maandamano bila kibali,
hatutangalia anatoka dini gani au chama gani hivyo polisi itafanya kazi
yake na kuwachukulia hatua kali,” alisema Kova na kuongeza:
“Kisheria kumtishia mtu siyo lazima utumie bomu, bali unaweza ukatumia kauli au vipeperushi kama hivyo vya maandamano.”
Alisema
wazazi watakaoruhusu watoto wa shule kufanya maandamano watachukuliwa
hatua za kisheria na kufikishwa mahakamani, ikiwezekana kufungwa mwaka
mmoja jela.
“Nimesikia wanataka kuwahusisha watoto wasiende shule,
ili wafanye maandamano ambayo yanazuiwa na sheria ya mtoto kutofanya
maandamano,” alisema Kova na kuongeza:
“Sisi tutahakikisha sheria
inachukua mkondo wake, kama kuna mtu amefikishwa mahakamani kuna
taratibu zake za kupata dhamana, siyo kufanya maandamano haramu.”
Pia, aliwaomba wananchi wasishiriki maandamano hayo kwani yataleta madhara makubwa kwa familia zao kwa wale watakaokamatwa.
“Hii
inajidhihirisha pale utakapotembelea familia za wale waliokamatwa
katika maandamano yaliyopita, watoto wanashindwa hata kwenda shule
kutokana na kukamatwa kwa wazazi wao na wanakosa nauli na chakula,”
alisema Kamanda Kova.
No comments:
Post a Comment