RAIS Jakaya Kikwete leo atahutubia mkutano wake wa kwanza wa hadhara
jijini Arusha tangu kumalizika kwa uchaguzi Mkuu mwaka 2010,
ulioshuhudia iliyokuwa ngome ya CCM, ikiangukia mikononi mwa Chadema.
Kikwete
ambaye ni Mwenyekiti wa CCM, atahutubia mkutano huo katika uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid, zikiwa ni siku nne tangu CCM
kinyang’anywe kiti cha Udiwani Kata ya Daraja II, kilichonyakuliwa na
Chadema.
Daraja II ni kati ya kata 29 zilizofanya uchaguzi mdogo
Jumapili iliyopita, huku CCM ikifanikiwa kutetea kata zake 24 na
kushuhudia tatu zikiangukia mikononi mwa Chadema iliyoshinda tano.
Mkuu
wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo alisema licha ya Rais Kikwete
kuhutubia mkutano wa hadhara, atazindua miradi ya miundombinu na elimu
katika Jiji la Arusha na Wilaya ya Monduli.
“Kabla ya kuhutubia
wakazi wa Arusha na vitongoji vyake, Rais Kikwete atazindua hospitali ya
Ortumer na baadaye kuwa mgeni rasmi sherehe za uzinduzi rasmi wa Arusha
kupanda hadhi kutoka manispaa kuwa jiji,” alisema Mulongo.
Alisema
Novemba 2, Rais Kikwete atakizindua rasmi Chuo Kikuu cha Teknolojia cha
Nelson Mandela kilichopo eneo la Tengeru wilayani Arumeru, baadaye
atatembelea kiwanda cha A to Z kinachotengeneza vyandarua vyenye
viuwatilifu vya kuua mbu.
Pia, ratiba hiyo inaonyesha Novemba 3,
atatembelea Wilaya ya Monduli ambako atazindua Sule ya Msingi Sokoine
kabla ya kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa barabara ya
Arusha Minjingu.
No comments:
Post a Comment