Monday, October 22, 2012

SERIKALI imesema inatarajia kuanzia mwakani kutoa waraka wa bei elekezi za ada kwa ajili ya shule binafsi ngazi ya awali hadi sekondari.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo, alipokuwa katika mahafali ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari ya Dk. Didas Masaburi.
Mulugo alisema katika bei hizo shule yoyote itatakiwa kutoza kiasi ambacho hakitazidi kile kilichowekwa na serikali na wale watakaokiuka amri hiyo watachukuliwa hatua za kisheria.
Aidha alisema kwa wale ambao itawabidi kwenda nje ya bei hizo itabidi kuomba kibali maalumu kwa Kamishna wa Elimu na ieleze ni vitu gani vya ziada ambavyo wanafunzi watavipata tofauti na shule nyingine.
“Haiwezekani mkate au aina ya vyakula vinavyoliwa na shule fulani ndio hivyo vinaliwa kwenye shule nyingine lakini ukija kwenye suala la ada mwingine iko juu. Lazima mtu atakayetaka kwenda nje na ada iliyopangwa aje na maelezo na tujiridhishe kabla hatujamruhusu kuipandisha,” alisema.
Hata hivyo katika bei hizo elekezi, Mulugo alisema zitaangalia pia na hali ya soko ikiwemo bei za vyakula ili pande zote ziweze kufaidika na sekta hiyo.
Mulugo alitumia fursa hiyo kuwataka wazazi kuhakikisha wanawapeleka watoto wao katika shule zilizosajiliwa ili kuepuka matatizo hapo baadaye ya kutofanya mitihani ya taifa.
Alifafanua kuwa watendaji wake hawawezi kuzunguka nchi nzima kukagua shule feki, hivyo ni wajibu wa wazazi kuhakikisha nao wanakuwa walinzi kwa kuepuka kuwapeleka watoto katika shule hizo na kutoa taarifa wanapobaini.
Naye mkurugenzi wa shule hiyo, Dk. Masaburi, alisema ili kuhakikisha kila mtoto anapata elimu bora ni vyema kusiwepo na michujo katika shule binafsi kwa kuwa hiyo ni haki ya kila mtoto.
Dk. Masaburi alisema pia watoto hao wanapaswa kutosogezwa darasa lingine pale wanapofeli ili kuepuka kuzalisha taifa la wasomi mbumbumbu.
chanzo tznzania daima

No comments:

Post a Comment