Mahakama ya kimataifa ya jinai
ICC hii leo inafanya kikao cha kwanza mbele ya umma dhidi ya mwanawe
aliyekuwa Rais wa Libya Muamar gaddafi,Saif Al Islam.
Saif anatuhumiwa kwa kuhusika na uhalifu wa kivita dhidi ya waasi waliopindua serikali ya babake mwaka jana.Hata hivyo tofauti zimeibuka kuhusu ikiwa kesi yake iendeshwe Libya au katika mahakama ya ICC mjini The Hague.
Mawakili wake wanatarajia kupinga pendekezo lolote la kesi yake kusikilizwa Libya wakisema kuwa hatapata hukumu ya haki nchini humo.
Hata hivyo maafisa wakuu nchini humo wanataka kesi yake iendeshwe nchini humo.
Katika siku ya kwanza ya kikao hicho, wakili wa Libya Ahmed al-Jehani ameitaka jamii ya kimataifa kuwa na uvumilivu akiwataka majaji wa mahakama hiyo kuelewa kuwa maafisa wa Libya wanahitaji muda zaidi kuweza kuandaa kesi ya haki dhidi ya Saif Gaddafi.
Bwana Jehani aliwaambia majaji kuwa hawajaondoa uwezekano wa mahakama ya ICC kuhusishwa katika kesi hiyo.
Hii ni mara ya kwanza mawakili wa mahakama ya ICC wameweza kukutana ana kwa ana na mawakili wa Libya mahakamani.
Hata hivyo maafisa wa Libaya wamekuwa wakisema kuwa hawako tayari kumkabidhi Saif kwa mahakama ya ICC na kwa hivyo lazima wawashawishi majaji kuwa Gaddafi atatendewa haki nyumbani.
Lazima waonyeshe kuwa wanafanya uchunguzi wao binafsi na wana nia ya kumfungulia Saif mashtaka sawa na yale ambayo yako kwenye kibali cha kumkamata ambayo ni ya uhalifu wa kivita.
No comments:
Post a Comment