Wednesday, October 31, 2012

Yanga yaikamata Simba

WAKATI mabingwa wa soka Tanzania Bara, Simba waking’ang’aniwa kwa sare ya 1-1 na Polisi Morogoro kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, watani zao Yanga walichanua Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam baada ya kuichapa Mgambo JKT kwa mabao 3-0 na kukabana kileleni zikipishana kwa tofauti ya mabao.
Simba iliyokuwa ikiongoza kwa pointi 22, ilijikuta ikianza kufungwa dakika ya 33, mfungaji akiwa Mokili Rambo ikiwa ni dakika tano tu tangu aingie kuchukua nafasi ya John Bosco, baada ya kuwatoka mabeki wa Simba. Matokeo hayo yalidumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili, Simba ilijitahidi kucharuka na kufanikiwa kuchomoa bao dakika ya 57, likifungwa na Amri Kiemba akiitendea haki kona ya Emmanuel Okwi. Hadi mpira unamalizika Simba na Polisi Moro ambao wanaburuza mkia katika msimamo wa ligi, walitoshana nguvu kwa sare ya bao 1-1.
Akizungumza baada ya mchezo, Kocha wa Simba, Mserbia Milovan Cirkovic, alilia na refa kutotenda haki, huku akidai licha ya wachezaji wake kupata nafasi nyingi za kufunga, alionekana wazi kuibeba Polisi.
Kocha msaidizi wa Polisi, Ally Jangalu alisema mechi ilikuwa nzuri na vijana wake wameongeza kiwango, kwani walikuwa wakisumbuliwa na ufungaji, lakini tangu walipocheza na Ruvu Shooting wamebadilika.
Simba: Juma Kaseja, Nassoro Masoud ‘Cholo’, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Amri Kiemba, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi, Mrisho Ngasa.
Polisi Moro: Aghaton Mkwando, Nahodha Bakari, John Bosco, Noel Msakwa, Hamis Mamiwa, Abdallah Mfuko, Bantu Adimini, Maige Paschal, Ally Shomari, Malimi Busungu, Nocolaus Kabipe.
Kwenye dimba la Taifa, Yanga ililianza pambano kwa uchu na dakika ya 2 tu, Nadir Haroub ‘Canavaro’ alitumbukiza kitu kambani kwa kichwa, akimalizia krosi safi ya Athumani Idd ‘Chuji’.
Yanga ilizidi kuliandama lango la Mgambo na dakika ya 39, Mrundi Didier Kavumbagu alikandamiza la pili akimalizia krosi murua ya Hamis Kiiza. Hadi dakika 45 zinamalizika, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi cha pili, Yanga ilizidi kucharuka na kuwapelekesha puta Mgambo hao wa JKT, ambako mtokea benchi, Jerry Tegete aliyepishwa na Kavumbagu, alipiga bao la tatu akiitumia vema kona ya Oscar Joshua dakika ya 79.
Dakika ya 86, Mgambo ilipata pigo baada ya mchezaji wake Salum Mlima kulimwa kadi nyekundu na mwamuzi Martin Saanya wa Morogoro kwa kumchezea vibaya Mbuyu Twite. Hadi mpira unamalizika Yanga 3, Mgambo 0.
Kwa matokeo hayo, Yanga na Simba zina pointi 23 kila moja, lakini Watoto wa Msimbazi wakifanikiwa kubaki kileleni kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Yanga: Ally Mustapha 'Barthez', Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Mbuyu Twite, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza, Haruna Niyonzima.
Mgambo JKT: Godson Mmasa, Salum Mlima, Yasin Awadh, Salum Kipanga, Bakari Mtama, Ramadhani Malima, Chande Magoja, Musa Ngunda, Issa Kandulu, Fully Maganga, Juma Mwinyimvua.
Matokeo mengine, huko jijini Arusha, Mtibwa Sugar ilizinduka na kuwalaza maafande wa JKT Oljoro kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, huku huko Mwanza, mechi kati ya Toto na Kagera ilishindwa kuchezwa baada ya mvua kubwa kunyesha, hivyo itapigwa leo.

No comments:

Post a Comment