ZAIDI YA 300 WASAINI KUPINGA MATOKEO,MAKONDA ANENA, AAPA KUTORUDI NYUMA
SASA
ni dhahiri kwamba matokeo ya uchaguzi wa Jumuiya ya Vijana ya Chama Cha
Mapinduzi (UVCCM), yameigawa jumuiya hiyo na huenda ikajikuta kwenye
mgogoro mkubwa wa kiuongozi ikiwa hatua za haraka hazitachukuliwa.
Hali
hiyo inatazamwa na baadhi ya wachunguzi wa mambo kwamba ni kutimia kwa
utabiri wa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete ambao aliutoa wakati
akifungua mkutano huo kwamba lazima viongozi watakaochaguliwa wachukue
hatua za kuondoa nyufa zitakazotokana na uchaguzi huo.
Kadhalika,
Rais Kikwete aliwaambia UVCCM kwamba watajuta ikiwa watachagua viongozi
wasio na uwezo kutokana na kushawishiwa na rushwa, kauli ambayo hata
hivyo, vijana hao waliipuuza kwani uchaguzi huo ulidaiwa kugubikwa na
vitendo hivyo hali iliyozua malalamiko kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa
mkutano.
Wasiwasi wa kupasuka kwa UVCCM unatokana na wanaodaiwa
kuwa wanachama wa jumuiya hiyo 379 wengi wakiwa wajumbe wa mkutano mkuu,
kusaini tamko la kupinga matokeo ya uchaguzi yaliyompa ushindi wa
nafasi ya mwenyekiti, Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi na Makamu
wake Mboni Mhita.
Kadhalika, hofu ya kukua kwa ufa huo, inatokana
na ukimya wa aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Paul
Makonda juu ya nafasi ya kuteuliwa kwake na Sadifa kuwa mjumbe wa Baraza
Kuu la UVCCM.
Tofauti na mgombea mwenzake, Rashid Simai Msaraka
aliyekubali uteuzi uliofanywa na Sadifa kumpa ujumbe wa baraza, Makonda
hadi sasa hajaukubali wala kuukataa, ukimya unaotafsiriwa kuwa unaweza
kuwa na ajenda kubwa ndani yake.
Hata hivyo, Makonda alipozungumza
na Mwananchi jana alisema atatoa uamuzi wake baadaye pale
atakapozungumza na vyombo vya habari kuhusu yaliyojiri katika uchaguzi
wa UVCCM.
“Kwa sasa siwezi kusema nimekubali uteuzi huu au hapana,
ninafanya hivi kwa sababu kama ulinisikia jana (juzi) nilisema uongozi
tuliouchagua ni aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa ni aina gani hiyo,
nitazungumza na baada ya hapo nitatoa sababu za kukubali au kukataa
uteuzi wa Sadifa,”alisema Makonda na kuongeza:
“Leo hii nikisema
nakubali uteuzi huo, basi wapo watakaosema nimehongwa au nimerubuniwa,
lakini pia nikisema naukataa wapo watakaosema nina uchungu wa kukosa
uongozi, sasa subiri tu siku nikisema nakubali au nakataa nitatoa
sababu”.
Gazeti hili jana lilipomtaka Makonda atoe ufafanuzi wa kauli yake
aliyoitoa juzi alisema: “Unawezaje kujivuna kwamba wewe ni mshindi
wakati dhamiri yako ikijua kwamba ulitumia hila, fedha na ulaghai,
huwezi kuwa na confidence (kujiamini) hata kidogo, sasa mtu asiyejiamini
hiyo ni fedheha.”
Kwa upande mwingine, kundi la vijana wanaoongoza harakati za kutaka
matokeo hayo yatenguliwe, jana liliwasilisha Makao Makuu ya CCM mjini
Dodoma, baadhi ya vielelezo kuhusu kuwapo kwa vitendo vya rushwa katika
uchaguzi huo.
Taarifa zinasema kundi hilo linaanda barua na
kiambatanisho cha majina na saini za wanachama wa UVCCM 379 ambao mpaka
sasa wamesaini tamko la kupinga matokeo ya uchaguzi huo kupeleka kwa
uongozi wa CCM.
Mmoja wa maofisa wa CCM makao makuu mjini Dodoma
ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe aliliambia gazeti hili kuwa: “Ni
kweli wale vijana wameleta sehemu ya ushahidi wao na tumeupokea, ila
tumewaelekeza kwamba lazima waandike barua ya malalamiko na iwe imefika
sehemu husika katika muda wa siku 14 tangu kutangazwa kwa matokeo”.
chanzo -gazeti la mwananchi
No comments:
Post a Comment