SERIKALI jana iliwasilisha tamko bungeni kurejesha kwa fao la kujitoa
katika mifuko ya jamii, ambalo liliondolewa na Mamlaka ya Kusimamia na
Kudhibiti Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Agosti mwaka huu.
Akiwasilisha
tamko hilo bungeni jana, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudencia Kabaka
alisema kwa kuzingatia mchakato ulioanza wa kuangalia upya sheria ya
mifuko ya hifadhi ya jamii, SSRA imeliondoa agizo la kuzuia mifuko kutoa
fao la kujitoa.
Alisema kufuatia hatua hiyo , mifuko yote
itaendelea kutoa fao hilo kama ilivyokuwa kabla ya zuio hilo na kwa
vigezo vilevile kwa wanachama wanaostahili kupata fao hilo.
Waziri
huyo alisema Serikali inaandaa muswada wa sheria wa kufanyia
marekebisho sheria ya mifuko ya jamii sambamba na kuondoa katika muswada
wa marekebisho ya sheria mbalimbali sehemu inayohusu fao la kujitoa.
Alisema
kabla ya kuandaa muswada huo, Serikali itafanya majadiliano na wadau
wote wakiwamo wabunge, vyama vya wafanyakazi, waajiri na wananchi.
Juzi SSRA ilitoa taarifa ya kufuta tamko lake la kuzuia fao la kujitoa kwa wanachama wa mifuko ya jamii nchini.
“Mamlaka ya Usimamazi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA),
inapenda kuufahamisha umma kufutwa kwa tangazo lililotolewa na mamlaka
Agosti 2012 kwenye vyombo mbalimbali vya habari lililohusu kusitishwa
kwa fao la kujitoa,” ilisema sehemu ya taarifa ya SSRA.
Pamoja na
maelezo hayo, taarifa hiyo pia ilieleza kuwa uamuzi huo unaendana
sambamba na hatua za Serikali za kuendelea na utekelezaji wa azimio la
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kikao cha nane
kilichoazimia pamoja na mambo mengine kuirejesha sheria ya hifadhi ya
jamii.
No comments:
Post a Comment