Thursday, October 25, 2012

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Bafana Bafana, Gordon Igesund, amesema timu yake tayari imefikia asilimia 75 katika maandalizi yake kupambana katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.


Bafana Bafana
Kocha wa Bafana Gordon Igelsund anasema timu hadi sasa imefikia asilimia 75 ya uwezo wake kamili
Afrika Kusini ni wenyeji wa mashindano hayo ambayo yatafanyika mwezi Januari mwaka 2013.
Bafana Bafana waliendelea kuonyesha uwezo wao, walipoishinda Kenya siku ya Jumanne, magoli 2-1, katika mechi ya kirafiki.
"Cha kunifurahisha hasa sio ushindi huo, bali ni kuhusiana na juhudi, namna walivyocheza, na mtizamo wa timu," alielezea Igesund.
"Bado hatujafika, kwani tunahitaji kucheza kwa pamoja - lakini vijana walionyesha uwezo wao."
Afrika Kusini ilitangulia katika mechi ya Nairobi kupitia Tokelo Rantie baada ya dakika 20, lakini Dennis Oliech aliweza kusawazisha kupitia penalti, na zikiwa zimesalia dakika 18 tu mechi kumalizika, kufuatia Bongani Khumalo kuunawa mpira.
Dakika nne baadaye, Bernard Parker ambaye awali alisaidia kutumbukiza wavuni bao la kwanza, alisaidiwa na Christopher Wekesa ambaye mpira ulipomgonga ulibadilisha mwendo na kuelekea wavuni na kuiwezesha Afrika Kusini kushinda.
Bao hilo la kujifunga wenyewe dakika ya mwisho linamaanisha kocha mpya wa Kenya, Henri Michel, ameanza kazi yake mpya kwa kushindwa.
"Ilikuwa ni ushindi uliopatikana kwa shida, na uwanja ulikuwa hauchezeki, lakini ni matatizo kama hayo ambayo yatatusaidia kimawazo," alieleza Igesund.
"Tulicheza kwa kuzingatia asilimia, na wala sio mchezo maridadi, katika kuwasukuma hadi wafanye makosa.
"Ninasikitishwa tu na bao ambalo tulifungwa, hatupaswi kuruhusu timu kutufunga magoli kama hayo. Lakini kwa jumla ilikuwa ni mazoezi mazuri, tukifikiria tulikusudia kufanya nini.
"Kwa sasa tumefikia asilimia 75 ya yale tunaweza kuyafanya."
Mwezi Januari, kwa mara ya kwanza, tangu fainali za mwaka 2008, itashiriki tena katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kutokuwepo katika mashindano ya mwaka 2010 na 2012.
chanzo bbc.com

No comments:

Post a Comment