Saturday, October 13, 2012

Serikali yashitakiwa The Hague,Mwanasheria mkuu ashangaa,wanasheria wengine nao waunga mkono.

MAUAJI ya mwandishi wa habari wa kituo cha runinga cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, na ya raia wengine yamezidi kuichafua Serikali ya Tanzania, na sasa imefunguliwa mashitaka katika Mahakama ya Uhalifu ya Kimataifa (ICC) iliyoko The Hague, Uholanzi.
Mbali ya mashitaka hayo yaliyopelekwa huko tangu Septemba 28, mwaka huu, Tanzania pia imeshitakiwa kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu.
Mashtaka hayo yalifunguliwa na Kituo cha Haki za Binadamu, ambapo Mkurugenzi Mtendaji wake, Hellen Kijo-Bisimba, alisema wamezitaka mamlaka hizo za kimataifa kufanya uchunguzi na kuichukulia hatua stahiki za kisheria Serikali ya Tanzania.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimechukua hatua hiyo kutokana na kuongezeka kwa mauaji ya raia wakiwa katika mikono ya vyombo vya dola, huku serikali ikigwaya kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika.
Hatua hiyo nzito na ya kwanza katika historia ya Tanzania, imekuja huku kukiwa na kusigana kwingi kwa ripoti ya serikali iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi na ile ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyoongozwa na Jaji Kiongozi mstaafu, Mussa Kipenka.
Wakati ripoti ya serikali chini ya Jaji mstaafu Ihema, ikionekana kuwatetea askari polisi waliohusika na mauaji hayo, na kusukuma lawama kwa chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ile ya Jaji Kipenka, imembebesha lawama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, kwa kuhusika na tukio hilo huku ikiisaficha CHADEMA.
Ripoti ya serikali ambayo imewachanganya Watanzania na wanasheria wengi, imedai kuwa "nguvu za kupita kiasi zilizotumiwa na polisi hazikusababisha kifo cha Mwangosi", lakini ikishindwa kuweka wazi kilichosababisha kifo chake kwa madai kwamba shauri hili liko mahakamani.
Hata hivyo, Ripoti ya Jaji Kipenka imeanika ukweli wote na kuwalaumu polisi, msajili wa vyama vya siasa na mamlaka za ulinzi na usalama za Mkoa wa Iringa kwa kukiuka misingi ya haki za kuishi, haki za kukusanyika na sheria ya sensa ambayo ilitumiwa na baadhi ya mamlaka kuzuia shughuli za CHADEMA.
Kadhalika, Ripoti ya Jaji Kipenka alisema wazi kuwa uchunguzi umebainisha kuwa CHADEMA walikuwa na haki ya kufanya shughuli zao za kisiasa kwa mujibu wa sheria na ilikuwa ni makosa kwa mamlaka kuwazuia kwa sababu za sensa.
Pamoja na hatua ya kushtakiwa kwa serikali katika mamlaka hizo za dunia, Bisimba alisema bado wanataka kuona viongozi wote wa serikali na vyombo vya dola waliohusika kwa namna yoyote na mauaji ya Mwangosi na raia wengine wakiwajibishwa.
Bisimba alisema hawaoni sababu za viongozi hao kutojiuzulu ama kuachishwa kazi na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Aidha, mkurugenzi huyo aliitaka serikali kuacha propaganda zinazotaka kuchochea vurugu katika taifa ambazo hazina tija na kutaka itambue kuwa sasa ni wakati wa mfumo wa vyama vingi, hivyo ni vyema ikaacha kutumia vyombo vya dola katika kuleta chuki na mafarakano katika jamii yanayohatarisha usalama na amani ya Watanzania.
Tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu mwaka juzi, kumekuwa na mauaji ya raia yenye sura za kisiasa, mengi yakitokea katika mikutano, maandamano na mikusanyiko inayofanywa na CHADEMA.
Vifo hivi ni vile vilivyotokea mkoani Arusha, Januari 5, 2011 ambapo watu watatu waliuawa kwa risasi na polisi katika maandamano ya CHADEMA, wilayani Igunga Novemba 2011, baada ya kada wa CHADEMA kuuawa kinyama na watu wasiojulikana na Arumeru Mashariki Aprili 2012 baada ya kuuawa kwa mwenyekiti wa CHADEMA wa Kata.
Mauaji mengine ni yale yaliyotokea Iramba Julai 2012, kufuatia kuzuka kwa vurugu katika mkutano wa CHADEMA ambapo kada mmoja wa CCM aliuawa, Agosti 27, 2012 mkoani Morogoro baada ya kuuawa kwa muuza magazeti na Septemba 2, 2012 mkoani Iringa kwa mwandishi Mwangosi.
Mwandishi akana kuhojiwa na Kamati ya Nchimbi
Katika hatua nyingine, mwandishi wa habari wa gazeti hili, Abdallah Khamis, amekanusha taarifa ya ripoti ya Kamati ya Nchimbi kuhusiana na kuhojiwa kwake.
Abdallah alisema kuwa yeye alipigiwa simu na mmoja wa wajumbe wa kamati ya Nchimbi akiambiwa ajiandae kukutana na kamati hiyo, lakini hakuitwa tena baada ya hapo.
Badala yake, alisema kuwa aliitwa na kuhojiwa na Kamati ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na kutoa maelezo yake.

No comments:

Post a Comment