Timu ya taifa, inayofahamika kwa jina Walias, ikicheza katika uwanja wa nyumbani wa Addis Ababa, siku ya Jumapili ilifanikiwa kuishinda Sudan magoli 2-0. Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 31 Ethiopia imeweza kufuzu kushirikishwa katika fainali hizo. Maelfu ya mashabiki wa Ethiopia walijitosa katika barabara za mjini Addis Ababa kufurahia ushindi huo, mara tu baada ya kipenga cha mwisho. Katika mechi ya mkondo wa kwanza mjini Khartoum, tarehe 8 Septemba, Ethiopia ilikuwa imelazwa magoli 5-3 na Sudan. Wakizungumza na kituo cha taifa cha televisheni, kocha wa timu ya taifa Sewnet Bishaw , na nahodha Degu Debebe, wote walisema ushindi huo ni kwa heshima za hayati waziri mkuu Meles Zenawi."Ushindi huu ni jambo la kupendeza mno. Ilikuwa ni shinikizo na wajibu mkubwa kweli. Kwa hiyo, kupitia uwezo wa Mwenyezi Mungu, matumaini ya raia wa Ethiopia yamejibiwa," alielezea Sewnet."Sisi kwa pamoja, wachezaji na vile vile mimi, tulikuwa tumeamua kwamba tukishinda tutamkabidhi marehemu waziri mkuu ushindi huo. Ninafurahia sana tumetimiza hilo.""Tangu alipotuondokea (Meles), tuliapa kuanzia wakati wa mazoezi yetu, kwamba tutamkabidhi ushindi huo,na nadhani Mungu ametuwezesha kushinda," alisema Degu.
Tajiri mmoja wa Saudi Arabia aliyezaliwa Ethiopia, Shaykh Muhammad Husayn al-Amudi, aliamua kuipa timu hiyo zawadi ya birr milioni tano, ambazo ni sawa na dola za Marekani 273,000.Licha ya Ethiopia kuwa miongoni mwa waanzilishi wanne wa shirikisho la Afrika la CAF, nchi ilipata ushindi tu mara moja, mwaka 1962, na imesubiri miaka 31 kufuzu kwa fainali hizo.
No comments:
Post a Comment