MKAZI wa Kijiji cha Kikwe wilayani Siha, Halima Munisi ametaka katiba
ijayo iitambue siku ya Ijumaa kuwa ni siku ya mapumziko kama zilivyo
siku za Jumamosi na Jumapili.
Munisi alitoa pendekezo hilo juzi
wakati akitoa maoni yake mbele ya kamati ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyokuwa ikiongozwa na Profesa Mwesiga Baregu.
Kwa mujibu wa
mwananchi huyo, Ijumaa kutokuwa ni siku ya mapumziko hasa kwa kuwa ndio
siku ya kumuabudu Mola kwa Waislam si sahihi na kutaka siku hiyo iwe ya
mapumziko.
Mkazi wa Kitongoji cha Nasai, Stanslaus Mallya alitaka
katiba ijayo iweke kifungu ili Mawaziri watakaoteuliwa katika Baraza la
Mawaziri wasiwe wabunge wa kuchaguliwa wala kuteuliwa.
Mallya
alisema kitendo cha Mawaziri kushika kofia mbili ya Uwaziri na Ubunge,
kinawafanya wasitekeleze majukumu yao ipasavyo hasa pale inapofikia
mahali pa kuibana Serikali.
Kwa upande wake mkazi wa Ndoroso,
Solomon Mmari alitaka Spika wa Bunge asiwe Mbunge na wala kuwa mfuasi wa
chama chochote cha siasa ili aweze kutenda wajibu wake kwa haki.
Hoja
hiyo iliungwa mkono na Radegunda Nyabu, mkazi wa Magadini Bomang’ombe
ambaye alisema endapo Spika anatokana na chama cha siasa, kuna kila
sababu ya kutoa upendeleo.
“Mbunge wa chama cha upinzani anatoa
mchango wake anaambiwa kaa chini hata kama ana mchango mzuri kiasi gani…
Spika akiwa kwenye chama fulani inaleta mpasuko”alisema.
Pia
alitaka Katiba Mpya iweke kifungu kitakachoilazimisha Tume ya Uchaguzi
(NEC), kutopanga siku ya uchaguzi kwa siku zile ambazo zinatumika
kumwabudu Mungu.
Kwa mujibu wa Nyabu, siku hizo ni Ijumaa kwa
waumini wa Kiislam na Jumamosi na Jumapili kwa waumini wa Kikristo ili
kila mmoja aweze kumwabudu na kumtukuza mola wake.
No comments:
Post a Comment