Wagombea wa
urais nchini Kenya katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao, watashiriki kwa
mara ya kwanza mdahalo wa urais kabla ya uchaguzi huo wa mwezi Machi
2013.
Hii leo baraza la vyombo la habari limezindua
mpango huo likilenga kuwaweka wazi wagombea wa urais mbele ya wananchi
kuweza kujibu hoja za wananchi kuwahusu, kitu ambacho hakijawahi
kufanyika nchini Kenya.Mijadala hiyo mitatu, itaandaliwa kwa ushirikiano wa vyombo vya habari chini ya baraza la vyombo vya habari na kupeperushwa moja kwa moja kupitia runinga, redio na kwenye mitandao, kuanzia Novemba 26.
Mdahalo mwingine utaandaliwa kabla ya duru ya pili ya uchaguzi wa urais, iwapo hapatapatikana mshindi katika raundi ya kwanza.
Mmoja wa waandaliizi wa midahalo hiyo ni afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni ya habari ya Nation, Linus Gitahi. Alielezea lengo la mijadala hiyo, " Kuna maswala kama vile elimu, usalama na miundo msingi. Tunataka kuwaleta wagombea hawa pamoja, ili wanachi wapate fursa ya kuwajua viongozi wao. Tunachotaka katika mijadala hii, ni watu watakaowaonyesha wakenya ni sera zipi walizonazo. Hatutazingatia wewe ni wa kabila gani, au wewe ni kiongozi wa kundi gani."
Huu utakuwa uchaguzi wa kwanza nchini Kenya, tangu uchaguzi mkuu wa 2007 uliokumbwa na ghasia zilizosababisha vifo vya zaidi ya watu 1,100 na maelfu wengine kuachwa bila makao.
Wagombea 13 tayari wameelezea azma ya kumrithi Rais Mwai kibaki ambaye anastaafu mwaka ujao baada ya kukamilisha mihula miwili ofisini.
Wagombea hao ni pamoja na waziri Mkuu Raila Odinga, makamu wa rais kalonzo Musyoka na naibu waziri Mkuu Musalia Mudavadi.
Naibu mwingine wa waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na Mbunge wa Eldoret Kaskazini William Ruto, ambao wanakabiliwa na mashtaka ya uhalifu wa kivita katika mahakama ya Kimataifa ya ICC, pia wameelezea azma ya kuwania kiti hicho cha urais, licha ya kesi inayowakabili.
Mashirika ya kijamii vilevile yamewasilisha kesi mahakamabni yakitaka Uhuru na Ruto kuzuiwa kuwania urais katika uchaguzi huo, wakisema hatua hiyo inakiuka katiba mpya ya Kenya.
chanzo bbc.com
No comments:
Post a Comment