Ukoo huo umehakikisha unashika nafasi zote za juu, ikiwamo ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo iliyokwenda kwa Shaibu Mtawa.
Mtawa alipata kura 811 na
kumshinda Mohamed Mrisho Kikwete aliyepata kura 613. Mtawa na Mohamed
wote ni ndugu wa damu wa Rais Kikwete.
Habari za uhakika kutoka miongoni
mwa wanachama, zinasema majina ya wanandugu hao yalipendekezwa kutoka
miongoni mwa wanachama 13. Wengi wao walikatwa kuanzia ngazi ya wilaya,
mkoa na kuhitimishwa kwenye vikao vya kitaifa ambavyo Mwenyekiti wake ni
Rais Kikwete.
Katika ngazi hiyo ya Taifa,
Mwenyekiti Kikwete alihakikisha majina matatu yanarejeshwa. Mawili -
Shaibu na Mohamed - yakiwa ni ya ndugu zake, na mwingine Omar Mhando.
“Mhando hapa aliwekwa kama
msindikizaji kwa sababu kwenye raundi ya kwanza aliangushwa. Kwa kuwa
hakuna mgombea aliyepata nusu ya kura, ikabidi upigaji kura urudiwe.
Ikawa hivyo kwa kupigia majina mawili ya ndugu.“Kilichofanyika kwenye uenyekiti
ni kuhakikisha majina mawili ya wanandugu hawa yanaingia ili mmoja
achaguliwe. Hilo limewezekana kwa kuchaguliwa Shaibu,” amesema mmoja wa
wanachama.
Habari za uhakika zinasema kwamba
kwenye uchaguzi huo kulikuwa na mvutano mkali kati ya wanandugu, hasa
kutokana na ukweli kwamba Shaibu ni mdogo wa Katibu Msaidizi wa Rais
Kikwete, Alhaji Kassim Mtawa.
“Mvutano ulikuwa mkali kweli kweli
bila kujali kuwa waliokuwa wakigombea ni wanandugu, ulikuwa mchuano wa
miamba,” kimesema chanzo chetu cha habari.
Baada ya uchaguzi huo, siku
iliyofuata wanandugu walikutana katika kikao cha ukoo, kwa ajili ya
kuzika tofauti zilizojitokeza miongoni mwao wakati wa uchaguzi.
Mohamed Kikwete anakaririwa kusema kwamba hakuwa na kinyongo kutokana na kushindwa na Mtawa.
“Aliyeshinda ni mdogo wangu, sina kinyongo,” alikaririwa akisema.
Baadaye kilifanyika kikao cha Halmashauri Kuu kwa ajili ya kumchagua Katibu Uenezi na Katibu wa Uchumi.“Kabla ya uchaguzi, wapigakura
kadhaa waliwekwa sawa, kuna kina mama walipata khanga, kina baba
wakapata misuli na fedha za usafiri. Wajumbe walikuwa kama 140.
Sikusikia aliyenung’unika kuwa amekosa kitu,” kimesema chanzo chetu.
Katika nafasi ya Katibu Uenezi,
mshindi alikuwa ni ndugu mwingine kutoka ukoo huo huo wa Kikwete,
aliyetajwa kwa jina la John Francis (Boli Zozo).
Kana kwamba hiyo haikutosha,
nafasi ya Katibu Uchumi Wilaya ya Bagamoyo akachaguliwa Iddi Swala. Huyu
ni mjukuu wa Rais Kikwete kwani amezaliwa na mtoto wa dadake Rais.
Ushindi wa Swala umezua gumzo
kubwa hasa kutokana na namna alivyokuwa kiongozi ndani ya Jumuiya ya
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Wilaya ya Bagamoyo. Mgombea aliyetajwa
kwa jina moja la Mtiga, aliyeelezwa kuwa na uwezo mkubwa wa uongozi,
alishindwa.
Awali, ndugu mwingine wa Rais
Kikwete aitwaye Yusuf Mrisho Kikwete, alishinda nafasi ya Mwenyekiti wa
CCM Kata ya Dunda, Bagamoyo.
Kuchaguliwa kwa wanaukoo hao,
pamoja na kupita bila kupingwa kwa Ridhiwani Kikwete ambaye ni mtoto wa
Rais Kikwete, kunaifanya Kamati ya Siasa ya Wilaya ya Bagamoyo iwe na
viongozi wakuu wanne ambao ni ndugu wa damu, pamoja na wajumbe wengine
wa kawaida. Nafasi hizo ni Mwenyekiti, Mjumbe wa NEC Taifa, Katibu wa
Uchumi na Katibu Uenezi.
Hata hivyo, kuwapo kwa wanandugu
hao kungeweza kupanuka zaidi endapo nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Bagamoyo, ingeshikwa na mwanaukoo
mwingine wa Kikwete, Magreth Halfan Kikwete. Magreth kaolewa na mtoto wa
Mzee Seleman Kikwete.
“Huyu wanachama wakasema
haiwezekani, wakaamua kumbwaga maana ilishaonekana sasa chama kinakuwa
cha ukoo tu. Tukaamua kumpa Hapsa Kilingo,” amesema mwanachama mwingine.
Kadhalika, ndugu mwingine wa Rais
Kikwete, Mwanaisha Halfani Kikwete, alipitishwa kugombea Ujumbe Baraza
Kuu/Halmashauri Kuu ya UWT Mkoa wa Pwani.
Wakati hali ikiwa hivyo kwenye
uchaguzi huu unaoelekea ukingoni, mtoto mwingine wa Rais Kikwete,
Khalfan Kikwete ni Mjumbe wa Baraza Kuu Idara ya Chipukizi ya Umoja wa
Vijana wa CCM (UVCCM). Mwenyekiti wa Idara hiyo ni Gabriel Makalla -
mtoto wa Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos
Makalla.
Ushindi wa Ridhiwani, Mama Salma
Kitendo cha Ridhiwani kupita bila
kupingwa kumeacha maswali mengi. Kuna habari kutoka kwa baadhi ya
wanachama kwamba wale waliothubutu kujitokeza kuwania nafasi hiyo
walitishwa, na wao wakatishika.
Wapo wanaosema kwamba kupita kwake
kwa mbinu hiyo kulitokana na hofu ya wajumbe kutokana na ukaribu
alionao na mzazi wake, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM Taifa.
Ni woga kama huo uliowaingia pia
wanachama na wapenzi wa CCM katika Wilaya ya Lindi Mjini, walioamua
kusalimu amri na kushuhudia mke wa Rais Kikwete, Mama Salma, akipita
bila kupingwa.
Ridhiwani na ubunge 2015
Watu walio karibu na kijana huyo wanasema kwamba anajiandaa kugombea ubunge Jimbo la Bagamoyo mwaka 2015.
Wanaotoa madai hayo wanatetea hoja
yao kwa kigezo cha namna Kamati ya Wilaya ilivyosukwa kwa kuwa na
viongozi wakuu ambao karibu wote ni ukoo mmoja. Wachunguzi wa mambo
wanasema matumaini ya Mbunge wa sasa wa Bagamoyo, Dk. Shukuru Kawambwa,
kuwania nafasi hiyo mwaka 2015 yamefutwa kutokana na kundi lake
kushindwa vibaya katika ngazi karibu zote.
Kwa sasa Dk. Kawambwa ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Jambo jingine ambalo JAMHURI
haijalithibitisha ni kwamba suala la ukabila nalo limekuwa likitawala
kwenye uchaguzi wilayani Bagamoyo, kama ilivyo kwenye uchaguzi wa CCM
katika maeneo mbalimbali nchini.
Dhambi hiyo ndiyo inayomfanya Dk. Kawambwa sasa aonekane kuwa ‘wa kuja” asiyetakiwa na “wazawa”.
Mbona hata Nyerere alipendelea?
Kuna hoja zinazojadiliwa kwenye
mitandao ya kijamii kwamba hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,
naye alipendelea ndugu zake wakati akiwa katika uongozi.
Anatajwa Joseph Warioba Butiku, aliyekuwa Katibu Myeka wa kiongozi huyo, kama kielelezo cha Mwalimu kuwabeba ndugu.
Pia anatajwa Joseph Nyerere,
ambaye ni tumbo moja na Mwalimu, aliyepata kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
kwa muda usiozidi miaka miwili; na pia Katibu wa Umoja wa Vijana wa
TANU.
Baadaye, kuanzia miaka ya 1970 hadi kifo chake miaka ya 1990, Joseph alikuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Butiama.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,
Jenerali David Musuguri, naye anatajwa kama mmoja wa waliopendelewa na
Mwalimu, ingawa kumbukumbu zinaonesha kuwa Janerali huyo alijiunga
katika Jeshi la Kikoloni la KAR kabla ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia
(1939-1945).
Chanzo: Jamhuri Media
No comments:
Post a Comment