Thursday, October 25, 2012

NSSF yazitaka Man U, Chelsea, Madrid KUWEKEZA HAPA NCHINI KATIKA MICHEZO

SHIRIKA la Hifadhi ya Jamii (NSSF), limeanzisha mchakato wa kujenga kituo cha kuibua vipaji vya soka nchini kwa kutumia jina la klabu mojawapo kubwa ya barani Ulaya.
Mkurungenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhani Dau, aliiambia Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC), jana kwamba, kwa sasa wapo katika mazungumzo na timu kubwa za Real Madrid ya Hispania, Manchester United, Liverpool na Chelsea za England.
Dk. Dau alisema katika mazungumzo na timu hizo, itakayokubali kuingia ubia, wataialika kuja nchini kuangalia eneo zuri la uwekezaji huo.
Alisema ubia huo utahusu namna ya kusaidia kufundisha jinsi ya kuwekeza katika mchezo wa soka na hatimaye vipaji viweze kuibuka na kuunda timu hapa nchini, itakayotumia jina la NSSF na timu watakayokuwa wameafikiana nao.
Dk. Dau alisema baada ya kuanzisha kituo hicho na kupatikana kwa timu hiyo, itakuwa ikipata faida ya kufunguliwa mafao yote ambayo yanatolewa na NSSF.
Na katika hatua nyingine, Dk. Dau alisema watafikiria kuwapa uanachama katika fao la bima ya afya, timu ya taifa ya soka Tanzania, Taifa Stars ili iweze kufanya vizuri zaidi.
Kauli hiyo aliitoa baada ya Mwenyekiti wa POAC, Zitto Kabwe, kuuliza kama Taifa Stars inapata fao hilo na kama haipati, je kuna uwezekano?

No comments:

Post a Comment