Tuesday, October 30, 2012

KUFUATIA CHAGUZI NDOGO ZA UDIWANI -CHADEMA Tumeshinda,Wasema Nape anapiga vuvuzela bila tathmini

WAKATI Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akitambia ushindi mkubwa walioupata katika kata 22 kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili, CHADEMA wamemtaka aache kuwa kama vuvuzela, wakidai wao ndio washindi.
Chama hicho kimesema kutokana na idadi kubwa ya kura walizopata katika kata zote hata zile ambazo hawakushinda ni dhahiri kuwa ngome yao inazidi kuimarika maeneo mengi nchini kiasi cha kuweza kuwanyang’anya CCM kata.
Kauli ya CHADEMA ilitolewa na Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha), John Heche, wakati akijibu tambo za Nape na kudai kuwa kada huyo ni sawa na vuvuzela, kwani kama angekuwa anafanya tathmini angeweza kubaini ni kwanini wananchi wanazidi kuikataa CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo Mtaa wa Lumumba, Nape alisema kuwa idadi kubwa hiyo ya madiwani waliyopata ni ishara kwamba CCM bado kinakubalika kwa wananchi na kitaendelea kushinda katika chaguzi zijazo.
Kauli ya Nape inakuja ikiwa ni siku moja tangu kumalizika kwa uchaguzi huo mdogo kwenye kata 29, ambapo CCM iliweza kurejesha kata zake 22 na kupoteza tatu zilizochukuliwa na CHADEMA iliyoshinda kata tano na CUF ikipata kata moja.
Nape alisema ushindi huo umetokana na chama hicho kuhubiri amani mara kwa mara katika mikutano yake, tofauti na vyama vingine ambavyo sera zao ni za kumwaga damu, kitendo ambacho wananchi hawakikubali.
“Ushindi huu unadhihirisha kuwa hata katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 chama chetu kitawashinda wapinzani,” alijigamba.
Nape aliponda opereshini ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) inayoendeshwa na CHADEMA nchi mzima, akidai inaandamana na vurugu na kwamba haitakisaidia chama hicho.
Alisema operesheni hizo zimekuwa zikisababisha vurugu na vifo katika maeneo mbambali kilipopita chama hicho.
“Juhudi zote walizofanya Katibu Mkuu, Dk. Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, hazikuzaa matunda, hiyo inatokana na siasa chafu za vurugu, hivyo wananchi wameamua kukinyima ushindi,” alisema.
Nape pia alisema kuwa CCM inalaani vurugu zilizotokea katika baadhi ya maeneo kulikofanyika uchaguzi huo kwamba huo si utamaduni wa Watanzania.
Alisema kuwa uchaguzi ulifanyika katika kata 29 na kati ya hizo 27 zilikuwa za CCM na mbili za CHADEMA, hivyo wao waliweza kuzirejesha kata zao na kutwaa nyingine tatu.
“Nape aache kupiga kelele kama vuvuzela bali wakae chini na kujifanyia tathmini, wajiulize ni kwanini watu wanazidi kuwakataa. Sisi kwanza tumeweka historia tangu mfumo wa vyama vingi uanze kwa kusimamisha wagombea kwenye kata zote, tumeweza kutetea kata zetu mbili na kuchukua za CCM tatu,” alisema.
Katika kujibu hoja hizo, Heche alisema kuwa wanachokifanya CCM sasa ni sawa na kufiwa na watoto halafu ukajipongeza kwa wale waliobaki, huku akibainisha kuwa uchaguzi huo umewawezesha CHADEMA kufika katika vijiji 116 na kusimika matawi.
Kuhusu madai ya Nape kwamba Operesheni ya M4C haikufua dafu katika uchaguzi huo kwa vile inachochea vurugu, alisema kuwa taarifa za magazeti mengi ya jana zilieleza bayana kuwa vitendo vya vurugu kwenye uchaguzi vilisababishwa na CCM kwa kuwashambulia wafuasi wa CHADEMA.
“CCM ni chama cha rushwa na wamechaguana kwa rushwa hata Mwenyekiti wao Jakaya Kikwete amekemea hilo kwenye mikutano ya UVCCM na UWT, sasa kwa mantiki hiyo Nape apime mwenyewe nani kapoteza na kama anafikiri tunafanya mzaha, basi angoje mwaka 2015,” alisema.

No comments:

Post a Comment