Thursday, October 18, 2012

Wajumbe CCM wapata ajali mbaya, mmoja afariki

UCHAGUZI wa Chama cha Mapinduzi (CCM), nafasi ya uenyekiti, mkoani Mwanza, jana uliingia dosari baada ya wajumbe kutoka wilayani Kwimba kupata ajali mbaya, ambapo wajumbe saba wamejeruhiwa vibaya huku dereva wa basi walilokuwa wakisafiria akifariki papo hapo.
Dereva aliyefariki ametajwa kwa jina moja la Mihayo, na kwamba ajali hiyo ilitokea katika maeneo ya Buhongwa jijini Mwanza katika barabara kuu ya kwenda Shinyanga.
Walioshuhudia waliieleza Tanzania Daima Jumatano kwamba ajali hiyo ilitokea majira ya saa 4:45 asubuhi, ambapo chanzo kinadaiwa kuwa dereva wa gari la mizigo aina ya Fuso alikuwa akigeuza gari lake katikati ya barabara.
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, wakati dereva huyo wa Fuso akigeuza katikati ya barabara, dereva wa basi la Bedui lenye namba za usajili T 853 BRB alishindwa kulikwepa Fuso kisha kuliparamia ubavuni.
Akizungumza na gazeti hili, muda mfupi baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, mmoja wa watu ambaye alikuwepo katika basi hilo, Shija Malado, alisema dereva wa gari la mizigo ndiye aliyesababisha ajali hiyo mbaya.
Aliwataja wajumbe walioumia vibaya kisha kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando ya jijini hapa (BMC), na kata zao kwenye mabano kuwa ni aliyekuwa mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Kwimba, Anthony Swagi (Mwagi), Elias Noninhale (Igongwa), Mohamed Yasin Fesa (Ngudu mjini), Shija Lutema (Mwamala), Adela Mayengela (Viti maalum), pamoja na Ofisa mmoja wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), katika wilaya ya Kwimba aliyetambuliwa kwa jina moja la Jilala, ambaye amevunjika mguu.
Shija alisema madiwani ambao mpaka sasa wako katika hospitali ya rufaa ya Bungando wakiendelea na matibabu ni Abel Mayenga, Feissa Yassin, Elias Nonitale, Shija Lutena, Martin Malecha pamoja na Anthon Swangisi.
“Watu wengine waliojeruhiwa vibaya ni pamoja na makondakta watatu waliokuwemo katika basi hilo, pamoja na ofisa mmoja wa TAKUKURU, Jilala. Huyu ofisa wa TAKUKURU yeye amevunjika mguu mmoja,” alisema Malando.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi, mkao wa Mwanza, Lily Matora, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, na kusema kuwa taarifa kamili zitatolewa baada ya askari waliofika eneo la tukio kukamilisha jarada.
chanzo tanzania daima

No comments:

Post a Comment