Waandishi Wetu, Dodoma
MMOJA wa Wenyeviti wa Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mussa Azzan Zungu pamoja na makada wengine wa CCM,
juzi usiku walikamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) mkoani Dodoma kwa tuhuma za rushwa.
Habari
zilizopatikana mjini hapa juzi usiku zinasema, Zungu alikamatwa saa 4.30
katika moja ya vituo vya mafuta akidaiwa kujaribu kutoa rushwa ya
Sh100,000 kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa Jumuiya ya Wazazi
wa CCM.
Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Dodoma, Eunice Mmari, jana
alikiri kuwakamata baadhi ya watu wakijihusisha na vitendo vya rushwa
akiwamo Zungu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake,
Mmari alidai kuwa vijana wake walimtia nguvuni Zungu juzi saa tatu usiku
katika Hoteli ya Golden Crown akiwa na wapambe wake wakiendelea kugawa
fedha kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Wazazi.
Alisema taarifa za Zungu
kudaiwa kugawa fedha hizo walizipata juzi mchana na kuanza kufuatilia
nyendo zake ambazo zilionyesha kuwa na dalili zote za rushwa.
“Tuliweka
mitego yetu kila mahali ndipo tukabahatika kukutana naye katika eneo la
hoteli hiyo akiwa na magari mawili, moja ikiwa ni teksi ya kawaida na
nyingine ikiwa ni Prado ambayo ndiyo ilisadikiwa kubeba pesa,” alisema
Mmari.
Kamanda huyo alidai kuwa kiasi cha fedha kilichokuwa
kikitolewa na Zungu kilikuwa Sh100,000 kwa kila mjumbe ili kumshawishi
ampigie kura.
Hata hivyo, alisema hawakuweza kumkamata moja kwa moja
akitoa na hata fedha hizo hawakuzikamata kwani maofisa wa Takukuru
walizingira gari dogo wakati fedha hizo zinasadikiwa zilikuwa katika
Prado ambalo baada ya vurugu hizo lilitokomea kusikojulikana.
Akizungumzia
madai hayo Zungu alisema: “Kwanza niseme kuwa si kweli kwamba
nimekamatwa nikitoa rushwa, nilikuwa katika kituo kimoja cha mafuta
wakaja watu ambao walisema wana shaka na gari langu.”
Aliendelea:
“Samahani, halikuwa gari langu, bali ilikuwa ni teksi, mimi
nikawaruhusu, wakaingia wakafanya ukaguzi na waliporidhika wakaniachia
nikaondoka.”
Taarifa za awali
Zungu alikuwa mmoja wa
wagombea wa nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) kupitia
Wazazi katika uchaguzi uliofanyika jana mjini Dodoma.
Habari
zilizopatikana mapema jana zilisema baada ya kukamatwa, Zungu alipelekwa
Ofisi ya Takukuru Mkoa wa Dodoma ambako alihojiwa hadi saa nane usiku
alipoachiwa baada ya kuwekewa dhamana na Mbunge wa Bukene (CCM),
Selemani Zedi.
Habari hizo zinaeleza kuwa baada ya kukamatwa, gari
alilokuwamo lilifanyiwa upekuzi kabla ya kupelekwa Ofisi za Takukuru,
pamoja na makada wengine wa CCM ambao walikamatwa kwa tuhuma hizohizo.
Kamanda
Mmari pia alithibitisha kukamatwa kwa makada wengine watano ambao
aliwataja kuwa ni Yahaya Danga, Busuro Pazi na Frank Mang’ati ambao
alidai kwamba walikuwa wakimsaidia Zungu katika mpango wake huo.
Mbali
na watu hao, Takukuru ilimtia mbaroni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi
Mkoa wa Mbeya, Fatuma Kasenga ambaye anadaiwa kukamatwa akitoa rushwa ya
chakula kwa wajumbe.
Alisema alikamatwa katika Hoteli ya Kitoli, Barabara ya Iringa saa tisa usiku.
Alisema kuwa watuhumiwa hao kwa pamoja waliachiwa kwa dhamana na kwamba uchunguzi unaendelea.
Katika
hatua nyingine, Mmari alisema kuwa taarifa walizokuwa nazo ni kuwa
mgombea wa nafasi ya Uenyekiti wa Jumuiya hiyo, Abdallah Bulembo alikuwa
akitoa rushwa zaidi.
“Tatizo ni kwamba wanazungumza lakini hawatoi
ushirikiano, maana kama wangetoa ushirikiano tungeweza kuwakamata kwa
urahisi,” alisema Mmari.
Bunge hawajui
Akizungumzia
kukamatwa kwa mbunge huyo, Mkurugenzi wa Shughuli za Bunge, John Joel
alisema Ofisi ya Bunge haikuwa na taarifa zozote kuhusu kukamatwa kwa
mbunge huyo.
“Ndugu yangu, ndiyo nasikia kutoka kwako, sisi hatuna
taarifa hiyo. Ni vigumu kuzungumzia jambo ambalo sijalisikia. Hata
hivyo, nakushukuru sana kwa taarifa,” alisema Joel.
chanzo mwananchi.
No comments:
Post a Comment