Lukuvi alimtangaza Mbunge wa Donge, Sadifa Juma Khamisi kuwa Mwenyekiti wa UVCCM baada ya kupata kura 483.
Sadifa
alimshinda Rashid Simai Msaraka aliyepata kura 263, wakati mgombea
mwingine Lulu Msham Abdallah licha ya kujitoa katika kinyang’anyiro
hicho muda mfupi kabla ya kura kupigwa, alipata kura nane.
Katika
nafasi ya Makamu Mwenyekiti Mboni Muhita alishinda katika duru ya pili
baada ya kupata kura 489 na kumshinda, Paul Makonda aliyepata kura 241.
Katika
duru ya kwanza, Mboni alikuwa amepata kura 361 na Makonda kura 206,
huku mgombea mwingine Ally Salum Hapi akipata kura 179. Uchaguzi huo
ulirudiwa baada ya wagombea wote kutofikisha nusu ya kura kama kanuni
zinavyotaka.
“Sheria kushindwa kwa heshima kuliko kushinda kwa fedheha.”
Makonda
aliyekuwa akizungumza kwa hisia jukwaani alisema ikiwa UVCCM wanataka
kujenga taasisi yenye nguvu na inayoaminika, lazima wahakikishe
wanajiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vinaua demokrasia.
“Uchaguzi
tulioufanya hatukumchagua Sadifa wala Mboni, bali tumechagua uongozi wa
aina ya jumuiya tunayoitaka, sasa tutarajie jumuiya hiyo…. kama
sikueleweka historia itakuja kutuambia maana ya maneno haya,” alisema
Makonda na kuongeza:
“Kama kuna mtoto wa maskini,
mtoto wa mkulima kama mimi amechagua au kupiga kura yake kwa sababu ya
rushwa, basi ajue amepanda mbegu maishani mwake.”
Baada
ya Makonda kutoa kauli hizo alishuka jukwaani na kwenda moja kwa moja
nje ya ukumbi ambako baadhi ya wapambe wake walimfuata na kuanza kulia
machozi.
Baadhi yao walisikika wakisema kwamba UVCCM
wameisaliti demokrasia kutokana na nguvu ya fedha. Hata hivyo, Makonda
alikuwa akiwafariji kwa kuwaambia wasife moyo.
WATUHUMIWA WAJITETEA HIVII
Kwa nyakati tofauti, wakijibu tuhuma hizo watuhumiwa wote
walikanusha kuhusika kutoa rushwa na kuwataka wanaolalamika kupeleka
ushahidi wao Takukuru na kufikisha malalamiko hayo katika vikao vya
ulinzi na maadili vya CCM.
Shigela kwa upande wake,
akizungumza na waandishi wa habari alisema kinachotokea sasa kuhusu
tuhuma hizo kilitarajiwa kwani ni kawaida watu wanaposhindwa katika
uchaguzi kutoa malalamiko hata kama hawana ushahidi wa tuhuma husika.
Shigela
alikanusha yeye na Malisa kutoa fedha kwa viongozi wa mikoa akisema kwa
nafasi yake asingeweza kupata fursa ya kufanya hivyo kwani alikuwa
mratibu mkuu wa uchaguzi kuhakikisha kila jambo linakwenda sawa.
“Kama
kuna watu hawakuridhika kuna taratibu za chama inabidi zifuatwe, kwa
mujibu wa taratibu zetu kuna siku 14 za malalamiko na hizo mtu anaweza
kuzitumia kuandika malalamiko yake na yapelekwe kwa viongozi wahusika
ili wachuke hatua,” alisema Shigela na kuongeza:
“Vinginevyo
taratibu za chama haziruhusu kutoa au kupokea rushwa kwa namna yeyote,
kwa hiyo kama mtu anadhani ana uwezo aitumikie jumuiya popote pale alipo
kwa sababu wote hatuwezi kuwa viongozi kwa pamoja.”
Kwa
upande wake, Malisa alisema: “Nimefanya kazi yangu na kutekeleza wajibu
wangu kwa ukamilifu, kama kuna jambo lolote ambalo linahusu UVCCM, basi
kamuulizeni mwenyekiti wa jumuiya maana yupo.”
Bashe
alikanusha kuhusika na vitendo vya rushwa na kuwataka wanaotoa madai
hayo, kama wana ushahidi waupeleke Takukuru au kufikisha suala hilo
katika vikao vya chama hicho.
“Waambieni kwamba
wasilete siasa za shule za sekondari UVCCM, maana kama wangeshinda ni
dhahiri kwamba wasingelalamika. Ninawapa ushauri wa bure, kwanza kama
wana ushahidi wa madai hayo kwamba mimi Hussein nimetoa rushwa, basi
wapeleke ushahidi wao Takukuru lakini pia ndani ya chama tunayo Kamati
ya Maadili na Usalama wapeleke malalamiko yao huko ili yafanyiwe kazi.”
Alisema hawezi kujihusisha na rushwa kwani hata Rais Kikwete katika hotuba ya ufunguzi alikemea vitendo hivyo.
Fredy
akizungumza kwa simu alisema: “Tuhuma hizo siyo za kweli kwani mimi
licha ya kwamba nilipata barua ya mwaliko wa kuhudhuria mkutano huo
sikuenda Dodoma kutokana na kubanwa na kazi.
“Kwanza
mimi si mjumbe wa mkutano mkuu japokuwa ni Katibu wa Uhamasishaji wa
Mkoa wa Arusha. Nilipata mwaliko lakini sikuweza kufika huko (Dodoma)
nimetingwa na kazi nyingi,” alisema.
No comments:
Post a Comment