MAMIA ya wakazi wa Arusha, leo wanatarajiwa
kujitokeza tena viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, kujua hatima
ya rufani ya kupinga kuvuliwa ubunge, Godbless Lema (Chadema) huku
kivutio kikitarajiwa kuwa mawakili ndugu, pande mbili tofauti kwenye
rufani hiyo.Mawakili hao, Tundu Lissu ambaye ameongezwa
kumwakilisha, Lema na kaka yake na Alute Mughwai anayewakilisha makada
wa CCM waliopinga ushindi wa Lema.Jaji Mkuu, Mohamed Othman
Chande akiwaongoza wenzake, Salum Masati na Natalia Kimaro,
waliahirisha kuanza kusikiliza rufani hiyo kufuatia kifo cha baba
mzazi wa mawakili hao.
Wakili Modest Akida wa upande wa
walalamikiwa, aliomba Mahakama ya Rufani kuahirisha kusikilizwa rufani
hiyo wiki iliyopita, kutokana na kifo hicho ambacho kilitokea Septemba
16. Tayari mazishi yamefanyika mkoani Singida Septemba 22, mwaka huu.
Hoja
hiyo ya kuomba kuahirisha usikilizwaji rufani hiyo hadi leo, iliungwa
mkono na wakili mwingine wa upande wa mrufani, Method Kimomogoro na
Wakili Mwandamizi wa Serikali, Vitalis Timoth anayemwakilisha
Mwanasheria Mkuu (AG).
Hata hivyo, Jaji Chande alisema ili
kuhakikisha rufani hiyo inasikilizwa kwa wakati, alitaka upande wa
mlalamikiwa kupeleka mahakamani pingamizi la hoja kuhusu rufani hiyo
kabla ya Septemba 26, mwaka huu na upande wa mrufani kujibu kabla ya
Septemba 28 sambamba na AG.
Mawakili wa pande zote, jana
walithibitisha kukamilisha taratibu za kujibu hoja, Wakili Lissu
aliwataka wakazi wa Arusha na maeneo ya jirani kuendelea kufika
mahakamani ili kujua hatima ya kesi hiyo.
“Nawaomba kesho (leo) mje
kwa wingi mahakamani kama ilivyo kawaida yenu, ili msikilize rufani ya
mbunge wenu Godbless Lema,” alisema Lissu.
Hata hivyo, baada ya
leo kusikilizwa hoja za pande zote na kama rufani hiyo ikiendelea,
shauri la msingi la kupinga hukumu ya Jaji Gabriel Rwakibarila kumvua
ubunge Lema itahamishiwa Dar es Salaam kutokana na kukamilika mkoani
Arusha vikao vya mahakama ya rufani.
Katika rufani hiyo, Mawakili
wa Lema wamewasilisha hoja 18 za kupinga kuvuliwa ubunge Lema, kutokana
na hukumu ya Jaji Rwakibarila ya Aprili 4, mwaka huu kukubaliana na
hoja za walalamikaji, Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo kuwa
Lema alitoa maneno ya kumdhalilisha aliyekuwa mgombea wa CCM, Dk
Batilda-Salha Burian.
No comments:
Post a Comment