Thursday, October 18, 2012

Haya ya Zanzibar nani alaumiwe?-Kwa nini hiki kikundi cha wahuni wanaofanya mauaji kisifutwe?

Zanzibar hali tete
Wakati Ponda kafikishwa mahakamani, visiwani Zanzibar hali bado ni tete kutokana na wafuasi wa jumuiya ya Uamsho kutanda mitaani na kufanya vitendo mbalimbali vya kutia wananchi hofu.
Ni katika vurugu hizo, askari polisi ameuawa kinyama kwa kupigwa mapanga kichwani na mikononi juzi wakati akirudi nyumbani kutoka kazini usiku wa saa 6 .30 eneo la Bububu Zanzibar.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Musa Ali Mussa, kwa waandishi wa habari, askari aliyeuawa ni F.2105 CPL Saidi Abdulrahman wa kikosi cha FFU Mkoa Mjini Magharibi.
Alisema kuwa inasadikiwa kuwa tukio hilo lilifanywa na wafuasi wa jumuiaya ya Uamsho ambayo imekuwa ikifanya vurugu mitaani tangu jana ikidai kuwa kiongozi wao Sheikh Faridi Ahmed Hadi ametekwa tangu Oktoba 16, mwaka huu.
Polisi walisema kuwa uchunguzi umeanza kumsaka kiongozi huyo ambapo ndugu yake mmoja, Saidi Omar Saidi, anahojiwa kwa vile ndiye aliyekuwa naye majira ya jioni wakati walipokwenda eneo la Mazizini kununua umeme.
Kwamba Sheikh Farid alimuamuru Saidi amuache katika eneo hilo aende nyumbani kupeleka umeme wakati akizungumza na watu aliowaita aliokuwa nao ndani ya gari aina ya Noah.
Aliongeza kuwa Saidi alikwenda na aliporudi tena, huo ukawa ndiyo mwanzo wa wafuasi wa Shekh Faridi kuanzisha vurugu wakitaka serikali imtafute.
Fujo hizo zilileta hasira ya kuchomwa na kuharibu miundombinu ya barabara, kuharibu maskani za chama tawala (CCM) za Kisonge na Muembe Ladu kwa kuzichoma moto.
Pia gari la zimamoto lilivunjwa kioo cha mbele, gari lingine la serikali lilivunjwa kioo cha pembeni, huku duka la pombe nalo likivunjwa na kuiba mali zilizokuwemo ndani.
Hadi muda huu watu kumi wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma ya makosa mbalimbali yaliyotokana na vurugu hizo. Upelezi wa kujua ukweli juu ya uvumi wa kutekwa Sheikh Faridi bado unaendelea.
Kwa siku nzima ya jana, hali ilikuwa si shwari visiwani hapa, askari walikuwa wakiranda katika maeneo yote ya mjini na kutupa mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya wafuasi wa uamsho.
Katika maeneo mengi shughuli nyingi za kibishara zilisitishwa na maduka kufungwa na wanafunzi kutolewa mapema shuleni.

No comments:

Post a Comment