Taarifa hiyo pia ilisema mtu aliyekuwa na Dk Ulimboka kabla ya kukamatwa
kwake alitambulishwa kwao na kigogo ambaye hakumtaja jina, kwa
makubaliano kuwa atakuwa anachukua madai ya madaktari dhidi ya Serikali.“Nathibitisha
kwamba mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye aliyenipigia simu na kuniita
kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye nilitekwa,” inaeleza taarifa
hiyo na kuonyesha namba za simu za mtu huyo anayedaiwa ni mfanyakazi wa
Ikulu.“Ninamfahamu sana bwana (jina tunalihifadhi kwa sasa),
kwa sababu alikuwa akitumwa mara kwa mara kuja kukutana na mimi na
tumekutana mara kadhaa kabla ya tukio lile. Nakumbuka alitambulishwa
kwetu na kigogo mmoja nikiwa pamoja na wawakilishi wengine wa
madaktari,” alisema.
Katika taarifa hiyo iliyoainisha namba
iliyokuwa inatumiwa na Dk Ulimboka kuwasiliana na mtu huyo, inaeleza pia
kuwa mpaka sasa mtu huyo yupo hai na kuwa yupo tayari kutoa ushirikiano
kwa chombo huru ili kuhakikisha haki inatendeka.Taarifa
inaeleza pia kuwa kwa nyakati tofauti mtu huyo alikuwa akitumwa kwa Dk
Ulimboka na mtu ambaye tamko hilo halikumtaja, lengo likiwa ni kuchukua
nyaraka mbalimbali na vyeti vya kuthibitisha taaluma za masomo yake.“Wale
wote waliotuhumiwa na ninaowatuhumu kunitendea unyama huu wako huru na
hakuna aliyeguswa. Je uhai na maisha yangu, yana thamani ndogo kama ya
mnyama anayekwenda machinjioni? alihoji Dk Ulimboka katika taarifa hiyo
na kuendelea:"Je Serikali ya nchi yangu itakubali lini kuundwa kwa tume huru kuchunguza unyama huu na kuhakikisha kuwa haki inatendeka?”
Dk
Ulimboka amesema katika taarifa hiyo kuwa: “Niko tayari kuhojiwa na
kutoa ushirikiano wangu kwa vyombo huru na makini vya uchunguzi ambavyo
vitaundwa ili kuweza kuubaini ukweli.”
Maelezo ya wakili wake
Akisoma
taarifa hiyo jana, Kicheere alisema kwa sasa Dk Ulimboka yupo nje ya
nchi kwa matibabu zaidi na aliandika tamko hilo mbele ya Wakili Nshala,
ambaye pia ameweka saini na mhuri wake.Hata hivyo, tamko hilo
ambalo Kicheere alilisoma mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es
Salaam jana, linaonyesha lilitolewa Oktoba 7, mwaka 2011, jambo ambalo
Nshala akizungumza na gazeti hili alisema ni makosa ya uchapaji.“Hilo tamko lilisomwa mbele yangu Oktoba 7, mwaka huu, hiyo ya kuandikwa mwaka 2011 ni makosa ya uchapaji tu.” alisema Nshala.Naye
Kicheere alisema, Dk Ulimboka yupo tayari kusema ukweli wote wa
kilichomkuta endapo itaundwa tume huru ya kuchunguza tukio hilo.
Alisema
taarifa ambazo alizitoa na kurekodiwa kwenye vyombo mbalimbali vya
habari ikiwamo mtandao ya kijamii, ni za kweli na alizotoa akiwa na
akili na kumbukumbu nzuri.Tamko hilo linaeleza kwamba, moja ya
uthibitisho kuwa taarifa hizo alizozitoa kabla ya kufika kwenye
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Kitengo cha Mifupa (Moi), na zile
alizozitoa akiwa hapo, ni kule kuweza kumwita na kumshawishi mtu
aliyemsaidia kutoka Msitu wa Pande.“Uthibitisho wa kumbukumbu
nzuri niliyonayo, ni pale nilipokutana na Juma Mganza katika Msitu wa
Mabwepande asubuhi ya siku ya tukio. Pamoja na maumivu makali niliokuwa
nayo kutoka kila sehemu ya mwili wangu, niliweza kumshawishi Mganza
kunifungua kamba za mikono nilizokuwa nimefungwa,” alisema Dk Ulimboka
na kuongeza;
“Pia kukumbuka namba ya simu ya rafiki yangu Dk
Deogratias ambapo Mganza aliweza kuitumia kuwasiliana naye kumpa
taarifa kuhusu tukio hilo. Ni kupitia taarifa hiyo ndipo suala la mimi
kufikishwa Moi lilipofikiwa.”Aliendelea: “Na kama niliweza
kukumbuka namba ya rafiki yangu, mambo hayo yanatosha kuthibitisha kuwa
ninachokisema ni ukweli na kuwa utimamu na kumbukumbu zangu ni sahihi”.
Usiku
wa Julai 26, mwaka huu, Dk Ulimboka alitekwa na watu wasiojulikana na
kupigwa vibaya ambapo Julai 27, alikutwa kwenye Msitu wa Pande uliopo
Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam.Baada ya tukio hilo, alisafirishwa mpaka Moi ambapo baadaye alipelekwa nje ya nchi kwa matibabu.
No comments:
Post a Comment