Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)
kimepokea fedha kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu
(HELSB) kwa ajili ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na wanaoendelea na
masomo chuoni hapo.
Taarifa hiyo ilitolewa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Utawala),
Profesa Yunus Mgaya, wakati akizungumza na NIPASHE chuoni hapo jana.
Alisema fedha za wanafunzi katika chuo hicho walianza kupokea kutoka
HESLB tangu juzi na kwamba, kinachoshughulikiwa kwa sasa ni kukamilisha
taratibu za hundi za fedha hizo.
Profesa Mgaya alisema wanafunzi wa mwaka wa kwanza watawahi kupokea
fedha zao endapo watawahi kusajiliwa mapema na kupewa kitambulisho cha
chuo na Jumamosi wiki hii wataanza kupokelewa rasmi chuoni hapo.
Alithibitisha kuwapo kwa uhaba wa hosteli kwa chuo hicho na kusababisha
wanafunzi kulala zaidi ya mmoja kwenye kitanda, ambapo pia alidai ni
makosa.
Alisema kwa sasa chuo kina zaidi ya wanafunzi 14,000, wakati kina uwezo
wa kutoa malazi kwa wanafunzi wasiozidi 6, 849 sawa na asilimia 49 na
kwamba, wanafunzi wa mwaka wa kwanza ndio wanaopewa kipaumbele.
Mkurugenzi wa Mawasaliano wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Rainfrida Ngatunga,
alisema fedha hizo hazijafika, lakini HESLB waliahidi wanazituma ndani ya wiki hii.
Afisa Habari wa Chuo Kikuu cha Waisilamu, Sudi Mndeme, alisema fedha za
malipo ya ada kwa wanafunzi zinapelekwa moja kwa moja katika uongozi wa
chuo, lakini za kujikimu wanaingiziwa wanafunzi wenyewe, hivyo hana
uhakika kama wameshapewa kwa kuwa chuo hicho kilifunguliwa jana.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (Taaluma), Profesa
Peter Gilla, alisema mpaka sasa kwao halijawa tatizo kwa kuwa chuo hicho
hakijafunguliwa na wanatarajia kufungua Oktoba 15, mwaka huu.
Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) cha jijini Mwanza kilisema
kinao wanafunzi zaidi ya 1,000, ambao uwapo wao chuoni hapo unategemea
upatikanaji wa mikopo kutoka HESLB.
Makamu Mkuu wa SAUT, Dk.Charles Kitima, alisema ingawa chuo hicho
kimeshafungua, lakini HESLB iliahidi kupeleka fedha baada ya Oktoba
Mosi, mwaka huu.“Ni kweli kwamba, serikali ilielekeza tusifungue vyuo kabla ya Oktoba
Mosi, lakini sisi ni chuo binafsi tuna mipango yetu. Ndio sababu
tulifungua tangu Septemba 25. Lakini kuhusu mikopo kwa wanafunzi,
tuliambiwa tusubiri hadi baada ya Oktoba Mosi,” alisema.
Hata hivyo, alisema ni mapema sana kuilaumu HESLB kwamba imechelewesha
fedha za mikopo kwa wanafunzi kwa sababu iliahidi kufanya hivyo ndani ya
mwezi mmoja baada ya Oktoba Mosi, mwaka huu.
Alisema kimsingi chuo hakiwezi kudai fedha hizo kutoka HESLB, badala
yake chuo kitawadai wanafunzi, ambao kama watacheleweshewa fedha hizo
ndio watakaoathirika.“Tuna imani bodi itazingatia ahadi yake ili wanafunzi wasiathirike iwapo
watacheleweshewa. Kimsingi wao ndio wanaopaswa kufuatilia sio sisi.
Lakini tunaamini mambo yatakwenda vizuri,” alisema.
No comments:
Post a Comment